KKKT yapongeza mchango wa Wahariri Walutheri kwa nchi

 

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa amesema anafuraha kuona KKKT linawatu wenye utaalam mkubwa, waadilifu na wanaoaminika kuongoza mashirika na taasisi mbalimbali za kihabari katika nchi.

Dkt. Malasusa ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Askofu Blaston Gaville katika warsha ya Wahariri wa Habari na Waandishi Waandamizi Walutheri iliyofanyika Luther House.

“Wapendwa wakristo wahariri na wanahabari, napenda mfahamu kuwa Kanisa linawatambua na kuheshimu kazi zenu katika ofisi mlizopo,” alisema Askofu Gaville na kuongeza,

“Hivyo na wapongeza sana naninatambua mchango wenu mkubwa katika jamii ya Watanzania, huku baadhi yenu mkiwa sehemu ya kundi kubwa la wanahabari ambao mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu mlikuwa na maandhimsho ya siku ya Uhuru wa Vyombovya Habari Duniani (WPFD) ambayo kitaifa ya lifanyika jijini Arusha.”

Pia, amesema Kanisa lingependa kufanyakazi na wahariri kwa ukaribu kwa kupokea mawazo, maoni na uzoefu wao katika mambo mbalimbali na hasa katika tasnia ya Habari na Mawasiliano.

“Ninyi mnaona mengi kupitia jicho la habari na mnaweza kulishauri Kanisa hususan katika kujenga taswira nzuri kwa wakristo na jamii kwa ujumla,” alisema Askofu Gaville.

“Kama mnavyo fahamu Kanisa kupitia Dayosisi zake linamiliki vyombo vinne vya Habari; Radio Sauti ya Injili-Moshi, Upendo Media Network-DSM, Utume Radio-Lushoto na Furaha Radio-Iringa. Kupitia vyombo hivi Kanisa limeweza kukusanya, kuhariri na kusambaza maudhui mbalimbali ikiwemo ya Kiroho na Kijamii kwa ajili ya uendelevu wa jamii ya Watanzania.”

Amesema anamatumaini kuwa kupitia kikao hicho, wataweza kuunda Jukwaa la Wahariri wa KKKT ambapo chombo hicho kitasaidia Kanisa katika kujadilina kuendesha vyombo vyake vya Habari na hasa katika masuala ya TEHAMA.

Ameongeza kuwa mara baada ya kufanya hivyo atazindua rasmi jukwaa hilo muhimu kwa maslahi makubwa ya Kanisa.

“Naamini warsha hii itakuwa mlango wa kuboresha masuala ya mawasiliano na habari ndani ya KKKT naitaendelea kuwa chachu ya habari za Kanisa kupewa kipaumbele katika mashirika mbalimbali ya habari hapa nchini,” alisema Askofu. Gaville.





Chapisha Maoni

0 Maoni