Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Maimbo
Mmdolwa amewahimiza Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na
kuongeza kuwa nchi inaweza kuingia katika mgogoro mbaya wa kikatiba kama
watasikiliza watu wanaotaka kuahirisha Uchaguzi Mkuu.
Askofu Mmdolwa amesema hayo Mei 11, 2025 jijini Mbeya katika ibada ya kuwekwa wakfu Canon Jacob
William Kahemele kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda
za Juu Kusini - Mbeya ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt.
Doto Biteko alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
“ Kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu uko hapa na tuliombe Taifa zima
kutoahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa tutaingia katika mtanziko
mkubwa na mgogoro wa kikatiba. Kama kuna changamoto zitafutiwe suluhu ziishe,”
alisema Askofu Mmdolwa.
Askofu Mmdolwa ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na
Taasisi za dini nchini na kuunga mkono Uhuru wa kuabudu ikiwa na lengo la
kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Akizungumza mara baada ya ibada hiyo, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema milango ya Serikali iko wazi
chini ya uongozi wa wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasihi wenye hoja
kujongea kwa mazungumzo.
"Ninachoweza kusema kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais,
wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu
unakuwa uhuru na wa haki huku nchi ikiendelea kuwa na amani.”
“ Uchaguzi utafanyika kwa uhuru na haki kama katiba
inavyotaka, waliposikika waliotaka marekebisho ya sheria Serikali ilipitia na
kufanya marekebisho ya sheria
zinazosimamia uchaguzi na leo milango ya
Rais Mhe. Dkt. Samia ipo wazi kwa yeyote mwenye kutoa malalamiko yake ili nchi
iende mbele,” amesema Dkt. Biteko.
Amewaasa Watanzania kuendelea kuiombea nchi ili amani
iendelee kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Biteko amesema
Serikali inathamini mchango wa madhehebu
yote ya dini, ikiwemo Kanisa la Anglikana. Katika nyanja za elimu, afya, maji,
na maendeleo ya jamii, Serikali inashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kwa
lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi.
Akitoa mfano wa
Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini yenye makanisa 37
yanayosimamiwa na parish katika mikoa ya Songwe na Mbeya kupitia makanisa hayo
yanasaidia kufikisha huduma ya kiroho kwa jamii.
“ Kuanzia mwaka 2016 hadi 2025 Kanisa kwa kushirikiana na
wadau limetumia zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendesha miradi ya
“Dreams na Archive” kwa kusaidia Elimu Maalumu ya Vitendo ya kujikomboa
Kiuchumi na Afya kwa Mabinti na Watoto wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI katika
maeneo ya Mbeya, Songwe na Tunduma,” amesema Dkt. Biteko.
Ambapo miradi hiyo imesaidia zaidi wananchi 160,000
waliokuwa na changamoto hizo za kijamii na kiuchumi. Aidha, imejiri zaidi ya
watu 150 hivyo kuwaongezea kipato na kuwarahisishia maisha wananchi.
Pia amesema Serikali itaendelea kushirikiana Kanisa la Anglikana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Dkt. Biteko amempongeza Askofu Kahemela katika
safari yake mpya ya kiutumishi huku akitoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo
kumtunza na kumsikiliza Askofu huyo pamoja na kumtia moyo kuwavumilia waumini
wake endapo changamoto zitatokea.
“ Tunakupongeza kwa moyo wa
kujitoa kwa Mungu, kwa utii wako kwa wito wa kiutumishi, na kwa maono yako ya
kiroho.”
Serikali inapenda kukupa uhakika kuwa tutaendelea
kushirikiana kwa karibu na Dayosisi hii chini ya uongozi wako, kwa lengo la
kukuza ustawi wa wananchi wetu, kulinda tunu zetu za taifa, na kuimarisha
mshikamano wa kijamii na kitaifa,” amebainisha Dkt. Biteko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mhe. Kapteni mstaafu George
Mkuchika amewaomba waumini wa kanisa la hilo kuwa na umoja na mshikano mara baada ya uchaguzi wa Askofu
wa Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini na kutii viongozi wa dini ili kuendeleza
kazi ya Mungu.
Aidha, amesema Serikali iliyopo ni sikivu na endapo kuna
malalamiko yasikilizwe, na kuwa Uchaguzi
usitenganishe Watanzania bali
uwaaunganishe, pia amewataka watu wenye
sifa za kugombea nafasi mbalimbali wafanye hivyo kwa kufuata utaratibu.
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mhashamu Askofu Sospeter
Ndenza amesema kuwa Askofu ni Kuhani Mkuu na Mchungaji Mkuu kwa niaba ya Kristo
na anasimamia nidhamu ya kanisa na kuona ibada zinasimamiwa na kufuata taratibu
za kanisa pamoja na kusimamia utoaji wa huduma za sakrementi tofauti.
Amesema wajibu huo ni
mzito unahitaji uongozi na hekima ya Mungu.
“ Jacob unahitaji kumuomba Mungu akupe hekima hasa katika
dunia ya leo, leo unapokusidia kuwekwa wakfu unahitaji hekima na adili ili
umwakilishe kristo,” amesema Mhashamu Askofu Ndenza.
Amesema Askofu huyo asiogope vitisho kwa kuwa kutakuwa na
watu watakao mpinga hata hivyo asitetereke badala yake ajue njia za Mungu na
asitumie akili zake bali ajinyenyekeze kwa Mungu naye atamsaidia.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya
Nyanda za Juu Kusini, Canon Jacob William Kahemele ameahidi kuwaombea viongozi
wa Serikali ili waweze kuiongoza nchi kwa amani na utulivu.
“ Wakati wa uongozi wetu tutahimiza sana watu kusali sana
ili kukua kiroho kwa kuwa shetani mjanja sana na anadanganya watu kufuata njia
za udanganyifu. Pia tutasisitiza sana uamsho wa kiroho ili watu wasiwe wachanga
na kuyumbishwa huku na huko,” amesema Askofu Kahemele.
Amesema wanaamini wameitwa kufanya majukumu makubwa kwa kutoa ibada, kutenda kazi kwa uaminifu sambamba na kusaidia wenye uhitaji.
Aidha, ametaja baadhi ya changamoto zinazowakumba vijana nchini za matumizi ya pombe kali,
sigara na michezo ya kamari hivyo ameiomba Serikali kuzuia uholela wa uuzaji wa
pombe kali na sigara.
Licha ya hayo ameipongeza Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati mfano treni ya kisasa (SGR) na kuiomba kufikiria namna ya kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Dar es salaam kwa kutumia treni hiyo ya kisasa ili kusaidia kukuza uchumi wa mkoa huo.
Ibada hiyo ya kumuweka wakfu Canon Jacob William Kahemele
kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania imehudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa
Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Akson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
0 Maoni