Jumuiya ya wanadiplomasia nchini imetakiwa kufikisha taarifa katika Serikali za nchi zao kuwa Dodoma ipo tayari na kwamba Serikali hizo zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi ya balozi kwenye viwanja vilivyotolewa bure kwenye mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud
Thabit Kombo (Mb) kwenye Mkutano maalum wa Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini
uliondaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kufanyika jijini Dodoma jana Mei
27, 2025.
Waziri Kombo
aliwaeleza Mabalozi hao kuwa siri kubwa ya mafanikio yoyote duniani ni kuwa na
imani na jambo unalolidhamiria
kulitekeleza. Serikali ya Tanzania tangu
ilipofanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma mwaka 1973
ilikuwa na imani na uamuzi huo na leo imani hiyo inatekelezwa kivitendo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya miundombinu na huduma za
kijamii ili kuuweka mji wa Dodoma katika mazingira mazuri ya kuishi, kwa watu
wa aina yote, wakiwemo Mabalozi.
Balozi Kombo alisema
kutokana na ujenzi wa mji wa Dodoma, fursa nyingi za uwekezaji zimeibuliwa,
hivyo ametoa wito kwa Mabalozi kuwaleta wawekezaji jijini Dodoma kuchangamkia
fursa hizo. Ametoa wito pia kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoa taarifa
ya kila hatua ya ujenzi wa mji huo kwa
wadau kwa lengo la kuwahamasisha kufanya uamuzi sahihi kuhusu Dodoma. Alisema
mkutano huo ni jukwaa muhimu la kupeana taarifa kuhusu maendeleo ya mkoa wa
Dodoma na kupendekeza uwe unafanyika kila mwaka.
Mwenyeji wa Mkutano
huo uliobeba kaulimbiu "Dodoma Ipo Tayari: Ipeleke Dodoma Duniani na Ilete
Dunia Dodoma", Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule alitumia
jukwaa hilo kueleza hatua mbalimbali zilizofikiwa katika ujenzi wa mji huo,
hususan katika maeneo ya miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji, umeme,
usalama, usafiri na burudani. Alusema huduma hizo zinapatikana kwa ubora wa
kimataifa, hivyo jumuiya ya
wanadiplomasia isihofie chochote inakaribishwa Dodoma na Dodoma ipo
tayari kwa ajili yao.
Mhe. Mkuu wa Mkoa pia
alibainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana jijini Dodoma katika
sekta za kilimo, utalii, logistics,
viwanda & ujenzi na madini na kuwakaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa
hizo.
Alisema Serikali ipo
katika mchakato wa kujenga Hombolo Thermatic Satelite City na kubainisha kuwa
hiyo ni fursa kubwa na adhimu kwa wawekezaji kushirikiana na Serikali
kufanikisha ujenzi wa mji huo.
Naye, Mwakilishi wa
Kiongozi wa Mabalozi ambaye alikuwa Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Isaac
Njenga alisema kuwa yeye na Mabalozi wenzake wameshuhudia hatua kubwa
iliyopigwa katika ujenzi wa mji wa Dodoma hasa baada ya kutembelea na kujionea
mji wa Serikali uliopo eneo la Mtumba, Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa na
ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato. Amesema kwa niaba ya
Mabalozi wenzake wameridhika na hatua iliyofikiwa na wameahidi kuzishawishi
Serikali za nchi zao kutenga fedha za kuanza ujenzi wa ofisi na makazi ya
balozi jijini Dodoma.
Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wapo jijini Dodoma kushiriki uwasilishaji
wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 tarehe 28 Mei 2025.
0 Maoni