Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa
Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa mchango wake katika sekta
za afya na elimu sambamba na kusaidia wahitaji jijini Mbeya.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Mei 10, 2025 jijini Mbeya
mara baada ya kukimbia mbio fupi za Tulia (Tulia Marathon) katika Uwanja wa
Sokoine.
“ Dkt. Tulia anafanya kazi kubwa kwenye sekta ya afya na
elimu pamoja na kuwajengea nyumba watu wenye uhitaji. Zile nyumba tunazoziona
anawakabidhi watu kumbe tayari kuna nyingine zimejengwa Uyole,” amesema Dkt.
Biteko.
Amesisitiza “ Nataka niwaambie hakuna sadaka kubwa kama kusaidia wahitaji na sisi
wengine tunajifunza kupitia wewe Dkt. Tulia”.
Ameongeza kuwa Dkt.
Tulia ni mtu anayejua kubuni vitu vyenye kuleta matokeo ambapo kupitia tukio la
Tulia Marathon amesaidia kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali.
Aidha, Dkt. Biteko amewapongeza washindi wa mbio hizo na
kuwashukuru wadau, wasanii na washiriki
wa mbio hizo, ambapo mwaka 2025 kumekuwa na
jumla ya washiriki 2,000 kutoka washiriki 307 mwaka 2017.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema
mbio hizo ni za kipee nchi nzima kwa vile wakimbiaji wanashiriki kwa siku mbili ili kutoa fursa kwao kushiriki
kikamilifu.
Amesema awali mbio hizo zililenga kusaidia sekta ya elimu na
afya pekee hata hivyo Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan imejenga shule na hospitali kwa wingi.
“ Kwa upande wa miundombinu hiyo, Serikali ya Dkt. Samia
imefanya kazi kubwa na zile fedha tulizokuwa tunapeleka katika sekta ya afya
sasa tunawakatia wananchi bima za afya, tayari tumekata bima za afya 9,000,”
amesema Dkt. Tulia.
Ameendelea kusema kuwa katika sekta ya elimu wamewapatia
madaftari na vifaa vya shule watoto zaidi ya 3,000 kupitia michango ya
washiriki wa wadau wa mbio hizo. Aidha, wamejenga nyumba tatu na zipo tayari
kwa ajili ya kugawa kwa watu wenye uhitaji.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amegawa zawadi kwa washindi wa msimu wa tisa wa mbio za Tulia.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni