Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Rachel Kassanda amewajulia
hali majeruhi wa ajali ya Bus la abiria aina ya Maning Nice lenye namba za
usajili T 848 ELA iliyotokea alfajiri ya jana Mei 7, 2025 katika eneo la Sululu
Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Akizungumza mara baada ya kuwaona majeruhi amesema ajali
hiyo imetokea alfajiri ya kuamkia leo ambapo bus hilo lilikuwa linatokea Dar es
Salaam kuelekea Tunduru na kwamba hakuna kifo kilichotokea na kuna majeruhi 23
ambao wapo Hospitali ya Mkomaindo na
baadhi yao wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Ndanda.
“Hongereni madaktari hatua ambazo mmezichukua zinatia moyo,
endeleni kupambana ili wote waruhusiwe salama waweze kuendelea na shughuli zao,”
amesema Mhe. Kassanda.
Mhe. Kassanda ametoa rai kwa wamiliki wa mabus kuhakikisha
wanakuwa na madereva wawili kwa nyakati za usiku ili kuepusha ajali
zinazotokana na uchovu wa madereva.
Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi Wilaya ya Masasi kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara wa kuhakikisha madereva wote wawili wanakuwepo kwenye
mabus yanayosafiri nyakati za usiku ili kuleta ufanisi wa safari na usalama wa
abiria.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Masasi Dkt. Salum Gembe
amesema hakuna kifo kilichotokea katika ajali hiyo na majeruhi wote wanaendelea
kupata matibabu katika Hospitali ya Mkomaindo.
“Tumepokea majuruhi 23, watoto 3 wa kiume, wanawake 9,
wanaume 11 ambao wameumia sehemu mbalimbali za mwili lakini Mungu amesaidia
hakuna kifo hata kimoja, wote wanaendelea na matibabu hapa Mkomaindo, mmoja tu
tumempa rufaa ya kwenda Ndanda Hospitali,” amesema Dkt. Gembe.
0 Maoni