TFS yakabidhi mbao na magogo kuunga mkono Sekta ya Elimu Kasulu

 

Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Kasulu, SCO Shadrack Msilu, amekabidhi mbao 250 na magogo 50 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo.

Hafla hiyo ilifanyika wiki hii katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, ikishuhudiwa na Kaimu Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, SCO Msilu alisema mazao hayo ya misitu yametolewa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu, hususan katika wilaya ya Kasulu.

“Tunatambua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu, hivyo TFS tunashirikiana na uongozi wa wilaya kuhakikisha kuwa wanafunzi wetu wanasoma katika mazingira bora,” alisema Msilu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu alishukuru kwa msaada huo na kuahidi kuwa mbao na magogo hayo yatalengwa moja kwa moja kwenye uboreshaji wa miundombinu ya shule, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa na samani za shule.

Chapisha Maoni

0 Maoni