OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) imewasilisha bungeni makadirio ya mapato kwa mwaka 2025/26
yenye takribani Shilingi trilioni 11. 783 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo
chini yake.
Bajeti hiyo imeongezeka
kutoka Shilingi trilioni 10.125
zilizotengwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Shilingi trilioni 11.783 na kuwa
na ongezeko la zaidi ya Sh trilioni
1.66.
Akiwasilisha makadirio ya
mapato na matumizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa
iamesema Shilingi trilioni 3.95 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo
ambapo kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 2.5 ni fedha za ndani, ikijumuisha
Shilingi bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri na Shilingi trilioni
1.45 ni fedha za nje.
Pia, amesema Shilingi
trilioni 7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara
Shilingi trilioni 6.3 na matumizi mengineyo Shilingi trilioni 1.53 ikijumuisha
Shilingi trilioni 1. 067 za mapato ya ndani ya halmashauri.
“Tumewasilisha si tu
makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini,
ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. TAMISEMI haitafuti sifa
ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida.”
Aidha, Mchengerwa ametoa
wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana,
kusonga mbele kwa mshikamano.
“Kwa dhamira hii, na kwa
imani kubwa katika maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi,
dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”
“Kwa hiyo, tunasema kwa
ujasiri mkubwa, TAMISEMI, ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Kila Shilingi ina
Jukumu, Kila Kiongozi ana Wajibu na Kila Mwananchi ana Nafasi!”
0 Maoni