WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ametoa maagizo kwa Mameneja wa Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara kwenye madaraja na makalavati yote ya barabara kuu
nchini ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na maji ya mvua.
Ametoa agizo hilo leo Jumatano (Aprili 16,
2025) alipokagua maendeleo ya ukarabati wa madaraja katika maeneo ya Matandu na
Somanga Mtama, Wilaya Kilwa Mkoani Lindi kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam -
Lindi yaliyokuwa yamekatika kufuatia mvua zinazonyesha nchini.
“Fedha ambayo tunatenga kwa
ajili ya ukarabati itumike ipasavyo kila baada ya mvua kubwa kunyesha
wakajiridhishe na kama kipenyo cha daraja na makavati yapo vilevile.”
Pia amemuagiza Meneja wa
Tanroads Mkoa wa Lindi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maeneo yote
yaliyoathirika na maji ya mvua yanatengenezwa na kuyarudisha katika hali yake
ya kawaida.
Amesema kuwa Serikali ina
mpango wa muda mrefu wa kujenga upya barabara ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara
kwa viwango, hivyo ujenzi wa madaraja ni hatua ya awali ya mpango mkakati huo.
“Tumetenga fedha ya ujenzi wa kilomita 100, tumefanya hivi ili kuepuka kuweka
viraka viraka badala yake tujenge upya eneo lote korofi.”
Kadhalika amewahakikishia
watumiaji wa barabara hiyo kwamba hakuna shughuli itakayo simama wakati
Serikali ipo na itaendelea kufuatilia mwenendo wa uimarishaji wa barabara hiyo.
“Lengo ni kuhakikisha, Serikali ipo kazini, na imeshaleta wakandarasi hii ni
kutokana na maelekezo ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa
amewahakikishia wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa Rais Dkt. Samia ametoa
fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vipande vilivyoharibiwa na mvua
zinazoendelea kunyesha.
Naye, Waziri wa Ujenzi,
Abdallah Ulega amesema kuwa mpaka sasa mkandarasi ameshaweka nguzo 23 kati ya
43 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu kwenye
eneo la Somanga.
0 Maoni