WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa kuridhia
Mashindano ya AFCON na CHAN kufanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa
kuendeleza na kukuza sekta ya michezo na utalii nchini.
Akizungumza
baada kukagua ukarabati na ujenzi wa Viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong
Zanzibar leo Aprili 7, 2025, Mheshimiwa Majaliwa amesema Watanzania watapata
fursa ya kuendeleza michezo na kuhamasisha wachezaji kufanya mazoezi zaidi ili
wapate sifa za kucheza michuano hiyo.
“Ujio wa
wageni wakati wa michuano utahitaji malazi, chakula na usafiri hivyo waliowekeza kwenye hoteli na vyombo vya
usafiri watapata faida kubwa na kujiingizia kipato, hii ni fursa nzuri ambayo
Marais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wametuletea kwa
sababu timu zinakuja na watu wengi.”
Aidha
Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na bora wa ukarabati wa
viwanja hivyo unaofanywa na kampuni za REFORM na ORKUN “Kampuni hizi zimetujengea
viwanja vilivyo na ubora unaokubalika”.
Mheshimiwa
Majaliwa ameongeza kuwa jukumu lililopo kwa sasa ni kuilinda miundombinu hiyo ili ubora uliofikiwa baada ya ukarabati uendelee kuwepo hadi
michuano hiyo itakapofanyika “Watanzania wanatamani kuvitumia viwanja hivi lakini wanatakiwa wajue kwamba
viwanja hivyo kwa sasa viko kwenye ukaguzi maalum unaofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika hivyo ni muhimu kuweka utarabu
ambao hautaathiri ubora ulipo”.
Pia amesema
kuwa pale inapobidi serikali hawatazuia viwanja hivyo kutumika katika michezo
mikubwa ila kinachotakiwa ni kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara baada ya
matumizi ili kulinda ubora wake utakaoiwezesha nchi kukidhi vigezo vya
kuendesha mashindano hayo .
Pia, Waziri
Mkuu amesema mashindano hayo yataleta manufaa makubwa katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya utalii na biashara. "Hii ni fursa nzuri ambayo Marais wetu Dkt.
Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wametuletea kwa sababu timu
zinakuja na watu wengi.”
Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na Katibu
Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ni miongoni mwa
viongozi waliombatana na Waziri Mkuu katika ukaguzi wa viwanja hivyo.
0 Maoni