Mawakili wa Serikali wametakiwa kutoa ushauri wa kisheria
unaozingatia maslahi mapana ya Serikali na Taifa ili kuiwezesha Serikali kuokoa
fedha zitakazosaidia kukuza uchumi kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Wito huo umetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally
Possi tarehe 24 Aprili 2025 wakati akizungumza na Mawakili wapya wa Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kwenye mafunzo elekezi yaliyotolewa kwa
watumishi hao yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na Mawakili hao kwa njia ya mtandao, Dkt. Possi
amesisitiza kuwa Mawakili wa Serikali wana jukumu la kutunza siri wakati wote
wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku katika uendeshaji wa mashauri ya
Serikali ili kulinda maslahi ya Serikali na kuleta heshima ya taaluma ya sheria
nchini katika kuhakikisha kuwa Serikali inapata haki yake katika kila shauri
linalofunguliwa dhidi yake au linalofunguliwa na Serikali dhidi ya watu wasio
na nia njema na Serikali.
Dkt. Possi alieleza kuwa OWMS ina jukumu kubwa la kuendesha
mashauri yote ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali. Hivyo ni muhimu kwa
Mawakili wa Serikali kufahamu vyema utamaduni wa Ofisi hiyo, muundo wake na
namna inavyotekeleza majukumu yake. Pia, amewasihi wajenge mahusiano mazuri na
taasisi nyingine zinazoshirikiana na OWMS mathalani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama.
Vile vile, amewataka wawe na utamaduni wa kufanya utafiti wa
kina wa kisheria kabla ya kuendesha shauri lolote la madai au usuluhishi ili
kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa utafiti unamuwezesha Wakili wa Serikali
kujenga hoja imara, kuelewa mazingira ya kisheria na kujiandaa vizuri wakati wa
usikilizwaji wa shauri.
Pia, amewasihi Mawakili hao kujenga tabia ya kujiendeleza
kitaaluma ili waweze kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi
katika maeneo maalum ya sheria mathalani sheria za kimataifa zinazohusu mafuta
na gesi na zinazovutia wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini kwa
lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, amewasisitiza wajiendeleze hasa katika mazingira ya
sasa ambapo sheria zinabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia ili waweze kuwa na maarifa ya kisasa na ujuzi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na
kwa kuzingatia maslahi ya umma.
Aidha, Dkt. Possi amewahimiza Mawakili wa Serikali kuwa na
nidhamu ya kazi kwa kuwahi kazini; kujenga mahusiano mazuri na watumishi
wenzao; na kuepuka kuwa kikwazo kwa wengine katika utekelezaji wa majukumu kwa
kuwa kuwahi kazini na kuwa na nidhamu ni misingi muhimu kwa watumishi wa umma
katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya
utumishi wa umma, kuboresha utendaji kazi kwa kujenga heshima, uaminifu na
ushirikiano mzuri mahala pa kazi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri na Udhibiti
Ubora wa Ofisi hiyo, ndugu Camilius Ruhinda amesema kuwa Mawakili wa Serikali
wapya wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu kubwa la kuendesha na kusimamia
mashauri ya madai na usuluhishi kwa mujibu wa sheria, weledi na kwa kuzingatia
utii kwa mamlaka, pamoja na kuheshimu viongozi wao muda wote na mamlaka ya
mahakama.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kuwa na
muonekano nadhifu wa mavazi na mwenendo unaoakisi taaluma ya sheria na Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali kwa ujumla.
Mafunzo hayo elekezi yamelenga kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kuhusu namna Serikali inavyofanyakazi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
0 Maoni