Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) limechangia huduma tiba na afya kwenye hospitali ya Jiji la
Berberati iliyoko katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati leo tarehe 14 Aprili
mwaka 2025.
Akizungumza mara baada ya
uchangiaji wa huduma hizo kwa niaba ya Kamanda Kikosi cha Nane cha Ulinzi wa
Amani nchini humo Luteni Kanali Theophil Nguruwe, Mkuu wa Operesheni na
Utendaji Kivita wa Kikosi hicho Maj. Mkangara Mzuma amesema kuwa JWTZ limefanya
hivyo ikiwa ni moja ya kuimarisha amani nchini humo.
"Siku zote JWTZ linathamini
maisha ya watu na linawajibika na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na
utulivu," alisema Maj. Mzuma.
Naye Mganga Mkuu wa
Hospitali hiyo, Daktari Sanzema Komoto amelishukuru JWTZ na uongozi wa Kikosi
Cha Nane Cha Ulinzi wa Amani nchini humo kwa moyo wao wa kujitolea ili
kurudisha amani kwa wananchi wake.
"Tangu JWTZ lianze
ulinzi wa amani nchini kwetu, limekuwa msaada mkubwa kwenye kusaidia huduma za
afya na wananchi wetu wamefaidika sana." alisema Daktari Komoto.
Huduma tiba na afya
zilizotolewa ni uchangiaji wa damu salama, vyandarua, vyakula, sabuni, maji
safi na salama pamoja na usafi wa mazingira ya hospitali hiyo.
0 Maoni