Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia
unapenda kuwajulisha kuhusu kuwepo kwa fursa za ufadhili wa masomo
(scholarship) nchini Indonesia kwa Watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika ngazi za Diploma, Shahada (Bachelor) na Shahada ya Uzamili
(Masters) chini ya ufadhili wa Serikali ya Indonesia kupitia mpango wake wa
Ufadhili wa Masomo wa The Indonesian AID Scholarship (TIAS) kwa mwaka wa masomo
2025/2026 katika fani mbalimbali.
Aidha, Serikali ya Indonesia itagharamia ada, posho ya kila
mwezi, bima ya afya, nauli ya ndege Tanzania-Indonesia-Tanzania, mafunzo ya
lugha na utafiti (Research) kwa watumishi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar watakaochaguliwa kushiriki katika mafunzo hayo.
Taarifa zaidi kuhusu uchaguzi wa fani (courses) pamoja na
vyuo zinapatikana kupitia tovuti ya
https://tias.kemenkeu.go.id/landing/. Aidha, waombaji watatakiwa
kuwasilisha maombi yao Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya nomination kabla au
ifikapo tarehe 04 Mei,2025.
Upatikanaji wa fursa hii adhimu kwa Tanzania ni sehemu ya mafanikio ya Ziara ya Kitaifa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nchini Indonesia mwezi Januari, 2024 pamoja na mazungumzo kati ya Mheshimiwa Dkt. Hussein A. Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Bw. Tormarbulang L. Tobing, Afisa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Indonesian Aid yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika mwezi September, 2024 Bali, Indonesia.
0 Maoni