Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.
Emmanuel John Nchimbi ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, kijijini Mwitongo na kukabidhiwa fimbo maalum na familia hiyo ya
mwasisi wa Tanzania na CCM.
Balozi Nchimbi ambaye yuko ziara ya kikazi ya siku tano
katika Mkoa wa Mara, mbali ya kukabidhiwa zawadi hiyo, yeye pamoja na msafara
wake, pia alipata fursa ya kuweka shada la maua na kufanya misa fupi kwenye
kaburi alipozikwa Mwalimu Nyerere.
Kiongozi wa Kabila la Wazanaki, Chifu Joseph Wanzagi,
alimwambia Balozi Nchimbi kuwa hicho ni kifaa cha kazi atakachotumia katika
dhamana alizoaminiwa kutumikia Watanzania. Alisisitiza kuwa huwa wanafanya
hivyo kwa kiongozi mwenye sifa zinazofaa.
“Tunakukabidhi fimbo hii. Huwa tunakabidhi kwa kiongozi
tunayemkubali. Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi utaitumia kuchapa na
kuwarekebisha wale wote ambao wanataka kutatiza shughuli za uchaguzi kinyume na
utaratibu wa Kikatiba,” alisema Chifu Wanzagi.
Balozi Nchimbi ambaye aliambatana na mwenza wake, Mama Jane Nchimbi, pamoja na viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama, pia alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Familia ya Mwalimu Nyerere, nyumbani hapo.
0 Maoni