Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka viongozi kote nchini kuweka maslahi ya wananchi mbele na
kuacha migogoro inayotokana na ubinafsi wao.
"Hawa Watanzania hawataki migogoro yetu sisi viongozi
na wakati mwingine migogoro tuliyonayo ni migogoro ya maslahi binafsi. Tumeacha
kuwahudumia wananchi tunashughulikiana, tunataka huyu akwame, huyu afanikiwe
kwa sababu tuna cartel (makundi)," amesema Dkt. Biteko
Akizungumza jana Aprili 24, 2025 Mundarara, Wilayani
Longido, Dkt. Biteko amesema kuwa amani ndiyo msingi wa utoaji huduma bora "Tunataka watu waungane, wafanye kazi ya
pamoja. Hakuna kitu kinachotia aibu kama unakuta kiongozi umepewa nafasi mahali
fulani ama wewe una cheo mahali fulani badala ya kuzungumza shida za watu
unawazungumza watu, Huyu kwako mbaya, yule mbaya, huyu mbaya, Wewe ukiulizwa
uzuri wako huna cha kuonesha."
Amesisitiza kuwa viongozi waliopata nafasi wanapaswa kumtumia mwananchi kama mteja wao wa kwanza, wa pili, na wa tatu "Viongozi tuliopata nafasi mteja wetu wa kwanza awe mwananchi, mteja wetu wa pili awe mwananchi, mteja wetu wa tatu awe mwananchi. Hawa wananchi ndiyo wanatupa uhalali wa sisi kuitwa viongozi, tukumbuke ni kwa kodi zao tupo hapa, Tusihubiri chuki. ” amesisitiza Dkt. Biteko.
0 Maoni