Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea
kufungua fursa za kiuchumi kwa kuboresha miundombinu na kuondoa vikwazo kupitia
mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara wilayani Longido
mkoani Arusha.
Meneja wa TARURA wilaya ya Longido, Mhandisi Lawrence Msemo ameeleza kuwa mradi
huo wa barabara ya Namanga - Sinonik - Mairouwa yenye urefu wa Km 9 na
makalavati madogo 10 una mchango mkubwa
kiuchumi kwa wakazi wa Mairouwa kwakuwa umerahisisha usafiri na usafirishaji wa
mazao na bidhaa kwenda mpakani Namanga.
Naye, Diwani wa Kata ya Ngarneibo, Mhe. Simon Ngarioi
ameipongeza serikali kwa kufanikisha uboreshaji wa barabara hiyo baada ya kuwa
na hali mbaya kwa muda mrefu.
“Naipongeza serikali kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hii
na kuwawezesha wananchi wa Ngarneibo hasa kiuchumi na kurahisisha kusafirisha
mizigo yao hadi Namanga, pia nahimiza wananchi kuitunza barabara hii ili idumu
kwa muda mrefu," amesema.
Bw. Elia Laizer mkazi wa Ngarneibo ametoa shukrani zake kwa
serikali kwa kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa manufaa yao.
"Tunashukuru kwa barabara, hapo awali palikuwa ni pori, watu walikuwa wanashambuliwa na wanyama, magari yalikuwa yanakwama, lakin sasa muda wa kwenda Namanga kuuza na kununua bidhaa umepungua.”


0 Maoni