WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 14, 2025 amezindua
msikiti wa Masjid Jaami’u Nuuril Hikma uliopo mtaa wa Yombo, Temeke jijini Dar
es Salaam ambao umejengwa na Taasisi ya Al-Hikma.
Akizungumza baada ya kuzindua msikiti huo, Mheshimiwa
Majaliwa ametoa wito kwa jamii na Watanzania watakaotumia msikiti huo kuutunza
kwani kufanya hivyo ni njia ya kudumisha uhusiano na Mwenyezi Mungu na
inahesabika kama sadaka.
“Mtume Muhamad S.A.W anatufundisha pia kutunza nyumba za
ibada, msikiti ni sehemu ya jamii na ni mahali pa ibada na umoja. Kupitia
hadithi ya Bukhari, ni wajibu wa waumini kutunza msikiti, kuhakikisha kwamba ni
sehemu safi, na inakidhi mahitaji ya ibada na mafunzo ya kiislamu.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa msikiti ni kituo
cha kiroho, kijamii, kiutamaduni na nyumba kwa ajili ya ibada na unatoa nafasi
kwa waumini kushirikiana katika ibada, kujifunza, na kujenga jamii bora kwa
kutoa huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa
viongozi wa dini kuliombea Taifa pamoja na kukemea vitendo vyote visivyo
mpendeza Mwenyezi Mungu.
“Tunajua mnaliombea Taifa hili, ila endeleeni kufanya hivyo
ili utulivu huu uendelee, tuachane na mambo yatakayoleta adha kwenye jamii,
tunafurahi mnavyohubiri amani na mshikamano, Mwenyezi Mungu analipenda Taifa
hili.”
Pia Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa
ujenzi wa msikiti huo. “Ujenzi wa Msikiti huu ni ishara ya juhudi za taasisi
hii katika kuimarisha misingi ya imani na maadili mema katika jamii”.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt Abubakar Zuber Ali Mbwana amesema kuwa maendeleo sio ugomvi bali ni kufanya mambo yanayoonekana na yanayompendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo ujenzi wa msikiti “fitna, ugomvi, fujo kwenye misikiti hatutaki, tupendane na heshima itawale.”





0 Maoni