Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii kwa mara ya
kwanza imepokea Faru weupe 17 kutoka kampuni ya AndBeyond ya nchini Afrika
Kusini kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi, utafiti na elimu katika
eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Akipokea faru hao katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika
kreta ya Ngorongoro tarehe 4 machi, 2025 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema mradi wa kuwaleta faru weupe Tanzania unalenga kuimarisha shughuli za
uhifadhi na kupanua wigo wa watafiti ambao kupitia faru hao watasaidia kutoa elimu kwa wananchi na hata wageni wenye lengo la kujifunza kuhusu maisha ya
wanyama hao.
Waziri Chana amebainisha kuwa faru hao 17 kutoka Afrika
kusini ni awamu ya kwanza ambapo awamu ya pili itahusisha faru wengine 19 na
kufikisha jumla ya faru 36 ambao watawekwa katika maeneo mengine ya uhifadhi
nchini.
Kamishna wa Uhifadhi
wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro
Dkt. Elirehema Doriye ameeleza kuwa faru ni miongoni mwa spishi zilizo
katika hatari ya kutoweka kutokana na vitendo vya ujangili na uharibifu wa
makazi yao hivyo kuletwa kwa faru weupe kreta ya Ngorongoro ni hatua muhimu ya
kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na kuhakikisha vizazi vijavyo vina fursa ya
kuwaona viumbe hao wa kipekee katika mazingira yao ya asili.
‘‘Ngorongoro tunajivunia kuwa moja ya maeneo machache barani
Afrika ambapo faru weusi wanaendelea kustawi, Kwa kushirikiana na taasisi za utafiti
za kitaifa na kimataifa, tumefanya
tathmini ya kina kuhakikisha Ngorongoro inakidhi mahitaji ya faru weupe ili
kuendelea kuimarisha uhifadhi,” alisema Dkt.Doriye.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro -NCAA Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) ameeleza kuwa, kuwasili kwa
faru 17 katika kreta ya Ngorongoro ni kuandika historia mpya kwa Tanzania kwani
itaongeza uhifadhi wa wanyama hao kwa kizazi kijacho.
Mabeyo ameeleza kuwa bodi ya wakurugenzi wa NCAA itaendelea
kuisimamia menejimenti ili kuweka kipaumbele katika usalama wa faru na
kushirikiana na wadau wa uhifadhi ili kuendeleza mikakati madhubuti ya
kupambana na ujangili hasa kutumia mifumo ya kutumia teknolojia za kisasa,
ikiwemo ufuatiliaji kwa drone, GPS tracking, pamoja na vikosi maalum vya doria
kuendelea kufanya kazi usiku na mchana.
Kwa upande wake mwakilishi wa viongozi wa mila kutoka nchini
Afrika Kusini, iNkosi Zwelinzima Gumede amebainisha kuwa lengo la kutoa Faru hao kwa Tanzania ni
kuendeleza juhudi za Uhifadhi na kuongeza uzalishaji wa spishi ya Faru weupe
katika nchi ya Tanzania pamoja na kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria
kati ya Tanzania na Afrika kusini ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela.
"Kabla ya kuleta Faru hawa hapa Ngorongoro watalaam
wetu walikuja kujiridhisha na Uhifadhi wa eneo hili na pia tumeona tafiti
mbalimbali zinaonyesha hifadhi hii ni Nyumbani kwa faru tena wakiwa katika
maeneo yao ya asili, hivyo hata faru hawa wapya tunaamini watakua vizuri na
kuzaliana kwa wingi,” amesema iNkosi Gumede.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, viongozi wa wilaya za Ngorongoro, Karatu na Monduli, Wadau wa uhifadhi kutoka kampuni ya AndBeyond nchini Afrika Kusini, bodi ya wakurugenzi wa NCAA na wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii.



0 Maoni