Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii
imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA) kwa hatua kubwa walizofanya
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Taifa
Tarangire ambayo itawezesha watalii wengi kufika kwa urahisi ndani ya hifadhi
hiyo.
Kamati hiyo imetoa pongezi hizo leo Machi 12, 2025, katika
ziara yake ya ukaguzi wa mradi wa Lango la kuingilia watalii la Mamire katika
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire pamoja na ukarabati wa barabara mbalimbali
zilizoko ndani ya hifadhi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava (Mb),alisema kuwa
miradi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii na kwamba kamati yake
itaendelea kufuatilia kwa karibu kasi ya utekelezaji wake.
Mnzava alisema kuwa “Tunaipongeza TANAPA kwa utekelezaji
mzuri wa miradi hii, tumeridhishwa na hatua ambazo zimefikiwa na tunaamini
miradi hii itakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa
kwa wananchi wa wilaya ya Babati.”
Aidha, Mnzava aliongeza kuwa TANAPA inapaswa kushirikiana
bega kwa bega na TARURA kuhakikisha kuwa barabara inayotoka Babati hadi Lango
la Mamire kuingia Hifadhi ya Taifa Tarangire inapitika vizuri ili kuongeza
urahisi wa usafiri kwa wageni hatua itakayochangia kuongezeka kwa idadi ya
watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Dunstan Kitandula (Mb), aliishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,chini ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kuimarisha
sekta ya utalii na kuongeza ushindani
katika soko la kimataifa.
“Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya utalii, tunaendelea
kutekeleza mikakati inayovutia watalii zaidi na kuongeza mapato ya taifa kwa
njia endelevu,” alisema Kitandula.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji,
alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa
kwa kasi katika sekta ya utalii hivyo TANAPA itaendelea kushirikiana na
serikali kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa
wananchi wa wilaya ya Babati na kwa taifa pia.
Mradi wa ujenzi wa lango la kuingilia wageni Mamire ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire umegharimu kiasi cha shillingi Billion 3.9 ikihusisha ujenzi wa Lango, vyoo, nyumba za kulala watumishi, kisima cha maji pamoja na mifumo mbalimbali ya umeme na unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi juni, 2025.





0 Maoni