WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa huduma jumuishi za
kifedha ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kuchochea
maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Amesema Serikali kwa kutambua hilo imedhamiria kuendelea
kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha sekta ya kifedha inazidi kuwa
jumuishi, fanisi, na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema hayo leo (Jumatatu, Machi 3, 2035) alipozindua
huduma mpya za kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika ukumbi wa
Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa katika vipindi tofauti, Serikali imekuwa
ikiandaa na kutekeleza mikakati ya Taifa ya kuboresha huduma jumuishi za
kifedha.
“Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023
- 2028 ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana kupitia Mpango Mkakati wa
Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha uliokamilika Desemba 2022.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jitihada
nyingine ni kuandaa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10 kuanzia mwaka
2024 hadi 2034. “Mkakati huu umeainisha malengo mahsusi ambayo kama nchi
tunaazimia kuyatekeleza ili kufikia uchumi wa kidijitali.”
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Sauda
Msemo amesema sekta ya fedha imeendelea kuwa na ustahimilivu na hivyo kuwezesha
shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika.
Aidha, Naibu Gavana huyo ametoa wito kwa taasisi zote za
kifedha zifuate viwango bora vya usalama wa mitandao na kugundua haraka pale
panapotokea udanganyifu wa aina yoyote.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema lengo la uzinduzi wa huduma hizo za NBC kidijitali ni kuboresha utoaji wa huduma za kifedha na kuzifanya zipatikane kwa urahisi. “Huduma hizo ni pamoja na ufunguaji wa akaunti, kuhamisha fedha, kupata mikopo bila ya kwenda katika tawi.”



0 Maoni