Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara
ya Maliasili na Utalii imevunja rekodi kwa kufikisha watalii milioni 5.3
(5,360,247) ambapo idadi ya watalii wa kimataifa 2,141,895 na watalii wa ndani
3,218,352 sawa na lengo lililojiwekea la kufikisha watalii milioni 5 ifikapo
2025.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) katika hafla ya kutangaza mafanikio katika sekta
ya utalii, iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
jana tarehe 31 Januari, 2025.
“Ninatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa na
uongozi wake thabiti uliotuwezesha kufikia hatua hii. Kupitia jitihada zake,
Tanzania imepata nafasi kubwa zaidi kwenye ramani ya utalii duniani, na
tunazidi kuona matunda ya kazi hiyo kila siku,” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, ameweka bayana kuwa bado Wizara yake ina wajibu wa
kuifikisha Sekta ya Utalii katika viwango vya juu zaidi ili kustahimili
ushindani katika soko la Kimataifa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana
na wadau wote wa sekta hiyo kuhakikisha inaendelea kuimarisha huduma, kuboresha
miundombinu, na kupanua masoko ya utalii ili Tanzania izidi kuwa kivutio
kinachopendwa zaidi duniani.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
nawapongeza na kuwashukuru wote mliochangia mafanikio haya. Kazi yenu ni ya
thamani kubwa, na tutaendelea kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha mafanikio
haya yanazidi kuimarika mwaka hadi mwaka,” amesema Mhe. Chana.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava ameipongeza Serikali chini ya Rais
Dkt. Samia Suluhu kwa kuwa na utashi wa kisiasa katika kuiendeleza Sekta ya
Utalii.
"Pamoja na kazi kubwa mnayoifanya na kufika malengo ya
ilani ni jambo kubwa sana lakini bado tuna kazi ta kufikia malengo kwenye
mapato tuko bilioni 4 na malengo ni bilioni 6," amesema Mhe. Mnzava.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi
amesema Wizara imejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa inatimiza lengo la
makusanyo ya dola bilioni sita za kimarekani na kuzidi ifikapo Desemba mwaka
huu.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Taasisi za Serikali, Mashirika binafsi na wadau wa utalii.
0 Maoni