Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan amewataka majaji na mahakimu wa Mahakama nchini kuhakikisha wanatekeleza
wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano ya kisheria na kikatiba, na kuwaasa
wasijifanye ‘miunguwatu’.
Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo Februari 3, 2025,
katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika viwanja vya
Chinangali Park, Dodoma.
Akifafanua neno la ‘miunguwatu’, Rais Samia akilihusisha na
binadamu wanaotekeleza wajibu wao kwa kujipa ukubwa unaofanana na ule wa
Mwenyezi Mungu, jambo alilosema watumishi wa taasisi za haki jinai na madai
hawapaswi kuwa nalo.
Kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu, ambayo mbali ya kutoa haki, ana kudra na jaala. Anaweza kuamua akupe au akunyime, alisema Rais Samia na kuongeza sasa hiyo ni kazi ya Mungu.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma,
amesema kuwa migogoro ya ardhi ndiyo chanzo kikuu cha jinai na changamoto
nyingi za kijamii na kiuchumi nchini, hivyo inahitaji uangalizi wa hali ya juu
katika Dira ya Taifa ya Maendeleo kufikia mwaka 2050.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa migogoro ya ardhi inaathiri
uwekezaji, biashara, mirathi na masuala mengine ya kijamii.
“Migogoro ya ardhi ni chimbuko la changamoto nyingi. Ikiwa
tutaweka mifumo bora ya usimamizi wa ardhi, tutapunguza migogoro mahakamani, na
mingi itaishia kwenye usuluhishi,” amesema Prof. Juma.
0 Maoni