Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi, amewasili nchini Namibia, akiongoza ujumbe wa CCM kwenye
mazishi ya aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Namibia na Baba wa Taifa hilo, Dkt. Sam
Shafiishuna Nujoma, yatakayofanyika tarehe 1 Machi, 2025.
Balozi Dkt. Nchimbi pamoja na msafara wake aliongozana nao,
ambao pia yumo Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano
wa Kimataifa, Ndugu Rabia Abdalla Hamid, aliwasili Uwanja wa Kimataifa wa Ndege
wa Hosea Kutako, jijini Windhoek, na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini
Namibia, Mhe. Mhe. Caesar Waitara, tarehe 26 Februari 2025.
Balozi Nchimbi atashiriki ratiba mbalimbali za utoaji wa
heshima za mwisho na kumuaga Dkt. Sam Nujoma, kuanzia tarehe 27 Februari 2025,
ambapo Chama Tawala cha Namibia, SWAPO, ambacho ni rafiki wa kihistoria wa CCM,
kimeandaa shughuli kwa ajili ya heshima ya mwasisi wake huyo.
Baada ya hapo, Balozi Nchimbi atashiriki ibada ya kitaifa ya
kumuaga Hayati Dkt. Nujoma iliyopangwa kufanyika tarehe 28 Februari 2025, kabla
ya shughuli ya mazishi ya kitaifa itakayofanyika tarehe 1 Machi 2025, katika
eneo la makaburi ya mashujaa, yaliyoko makao makuu ya nchi hiyo, jijini
Windhoek.
Uhusiano kati ya Namibia na Tanzania, halikadhalika CCM na
SWAPO na watu wa nchi hizo mbili, ni wa kihistoria, ukiwa umejengwa katika
misingi imara tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru dhidi ya wakoloni na
makaburu.
Itakumbukwa kuwa Hayati Dkt. Nujoma na viongozi na wanachama
wengi wa SWAPO na Namibia waliishi maeneo mbalimbali uhamishoni nchini
Tanzania, tangu miaka ya 1960, wakishiriki mapambano ya kupigania uhuru wa nchi
yao, ambako pia ndipo walipoanzisha Chama cha SWAPO ili kuendesha shughuli za
kuikomboa nchi yao kisiasa, hadi walipopata uhuru mwaka 1990.
0 Maoni