Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linashiriki
Maonesho ya Utalii ya (Outbound Travel Market) OTM 2025 kwa lengo la kunadi
vivutio vyake vilivyopo ndani ya Hifadhi za Taifa 21 zinazopatika nchini
Tanzania.
Licha ya kutangaza vivutio hivyo pia TANAPA itajikita
kuelezea fursa za uwekezaji zilizomo ndani ya hifadhi hizo na kuwahamasisha
wawekezaji kuja kuwekeza katika malaza, mazao ya utalii na katika sekta ya
usafirishaji ambazo ni injini katika kukuza sekta ya utalii.
Maonesho hayo yanayowakutanisha pia mawakala wa usafirishaji
wa ndege kutoka Marekani, Ulaya na Asia yameanza jana Januari 30, 2025 na
yanatarajiwa kuhitimishwa Februari Mosi, 2025 huku kwa upande wa TANAPA
ikiwakilishwa na Maafisa Utalii kutoka Makao Makuu ya Shirika na Hifadhi za
Taifa Kilimanjaro na Mikumi.
TANAPA inatambua kuwa India ni soko linalokua kwa kasi
katika utalii wa kimataifa kutokana na wingi wake wa watu na inaendelea
kuchipukia katika teknolojia. Kwa kutambua hivyo TANAPA imeona ni vyema kutumia
nafasi hii ya maonesho kutangaza vivutio vyake.
Sambamba na maonesho hayo pia, TANAPA imeandaa kampeni ya
kutangaza vivutio vyake kupitia “Roadshow” katika miji ya Delhi, Chennai, na
Bengaluru. Vilevile, TANAPA imepanga kukutana na mawakala wa utalii na
usafirishaji ili kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na
India.
0 Maoni