Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi
(DCP) Wilbroad Mutafugwa leo Januari 22, 2025 katika Chuo cha Polisi Wanamaji
Mwanza (MPC) kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania amekabidhi Bendera
ya Taifa kwa Kikosi Maalum cha Mbinu na Silaha (SWAT) kinachokwenda nchini
Rwanda kwa ajili ya mashindano ya Vikundi Maalum vya Kupambana na Ugaidi.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia tarehe 23 hadi 30
Januari 2025 na yatahusisha matukio matatu ambayo ni Mapambano ya Karibu
(Assault event), Ulengaji Shabaha (Tactical event) na vikwazo (Obstacles)
ambapo jumla ya nchi 14 za ukanda wa EAPCCO zinatarajiwa kushiriki.
Aidha, mashindano hayo yatapamba Mkutano Mkuu wa Wakuu wa
Majeshi ya Polisi wa nchi za Mashariki ya Afrika (AGM) ambao unatarajiwa
kufanyika nchini Rwanda kuanzia tarehe 27.01.2025 hadi tarehe 29.01.2025.
Akikabidhi bendera ya Taifa ya Tanzania kwa kikosi hicho
kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Mutafungwa amewakumbusha
washiriki wa mashindano hayo kuwa Taifa linawatazama hivyo wajitahidi
kuliwakilisha vyema na kurudi na ushindi huku wakizingatia kauli mbiu ya Jeshi
la Polisi ya Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu.
Hata hivyo, Kamanda Mutafugwa mbali na kuwatakai kila la
heri, amewataka kwenda kujituma zaidi kwani hakuna mafanikio bila kujituma
sambamba na kuongeza ushirikiano miongoni mwao na washiriki wengine.
"Jeshi la Polisi ni taasisi kubwa na limejijengea
heshima kubwa ndani na nje ya nchi, sisi hatuna wasiwasi tunatarajia kuona
mnarudi na ushindi hivyo mnatakiwa kuongeza morari," amesema Kamanda
Mutafungwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa kikosi hicho maalum
Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Aizack Mwakisisile amesema yeye pamoja na timu
yake wamejiandaa vizuri na wanamatumaini makubwa ya kurejea nchini
wakiwa na ushindi.




0 Maoni