Mwanaharakati Maria Sarungi atekwa Nairobi Kenya

 

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema kuwa mwanaharakati na mhariri wa kujitegemea wa Tanzania Maria Sarungi ametekwa nyara akiwa nchini Kenya.

Katika taarifa kupitia mtandao wa X, shirika la Amnesty International limesema kwamba Maria alitekwa na wanaume watatu waliokuwa na silaha na ambao walikuwa na gari nyeusi aina ya Noah.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa tisa na robo mchana katika eneo la Chaka Place, Mtaa wa Kilimani Jijini Nairobi.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Irungu Houghton ameiambia BBC kuwa wako katika eneo la tukio wakijaribu kupata taarifa zaidi.

Hii si mara ya kwanza raia wa kigeni kutenkwa nchini Kenya.

Mwezi Novemba mwaka jana, mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Dkt. Kizza Besigye alitekwa Jijini Nairobi na watu wasiojulikana na kurejeshwa nyumbani kwao nchini Uganda na kufunguliwa kesi.

Pia, wakimbizi wanne raia wa Uturuki nao walitekwa na kutimuliwa nchini Kenya kwa lazima na kupelekwa hadi Ankara, ambako walikabiliwa na tuhuma za kula njama dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdogan.

Chapisha Maoni

0 Maoni