Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imehitimisha kambi
ya upasuaji wa upandikizaji figo kwa kuwapandikiza wagonjwa watano ambapo figo
imevunwa kutoka kwa wachangiaji kwa kutumia njia ya kisasa ya matundu (Hand
Assisted Laporascopic Donor Nephrectomy).
Kwa mujibu wa Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Immaculate
Goima kambi hiyo iliyochukua takribani siku tatu kuanzia Januari 29 hadi 31,
2025 imehusisha wataalam wa ndani ambao wameshirikiana na wataalam kutoka Korea
Kusini.
Dkt. Goima amesema kutokana na utaalam uliotumika kuvuna
figo kutoka kwa wachangiaji imewafanya wachangiaji hao kukaa hospitalini kwa
muda mfupi ambapo watakaa wodini kati ya siku mbili hadi tatu na kuruhusiwa
kurejea nyumbani kwao kuungana na familia zao.
Dkt. Goima ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji uliofanywa
na Serikali wa kusomesha wataalam, kununua vifaa tiba, vitendanishi na kujenga
uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali duniani kumesaidia kutoa huduma hizi za
ubingwa bobezi hapa nchini kwa weledi na ubora wa hali ya juu.
Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila ndio hospitali pekee
hapa nchini inayotumia utaalam wa kuvuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia
njia ya matundu madogo, baada ya upandikizaji huo hospitali hiyo inafikisha
idadi ya wagonjwa 16 waliopandikiza figo tangu huduma hiyo ilipoanza kutolewa
Muhimbili Mloganzila Aprili, 2023.
0 Maoni