Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi
walioko kwenye maeneo yenye Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza
Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wametakiwa kutokuhifadhi maliasili peke
yake bali na miundombinu inayoendelea kuboreshwa kwenye hifadhi za Taifa.
Wito
huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dunstan
Kitandula alipokuwa akiongea na viongozi wa Kanda ya Kusini na hifadhi ya Taifa Ruaha alipokuwa katika
ziara ya kukagua miradi inayojengwa chini ya ufadhili wa mradi wa Kuboresha
Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Mhe. Kitandula alisema kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya jitahada kubwa za
kutangaza sekta ya utalii kupitia Filamu za Tanzania The Royal Tour na Amazing
Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii, hivyo kama wahifadhi hatuna budi
kutimiza wajibu wa uhifadhi wa maliasili na vivutio vya utalii vilivyopo
ikiwemo kuhifadhi miundombinu inayojengwa katika hifadhi mnazozisimamia.
Aidha, Mhe. Kitandula hakusita kuwaonya na
kuwakumbusha watumishi wanaofanya kazi katika kampuni zilizopata kandarasi ya
kujenga miundombinu hiyo kuwa wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha miradi
hiyo inajengwa kwa kufuata mikataba iliyowekwa na kutokujengwa chini ya viwango
kwa kuwa miradi hii ni ya watanzania wote.
Mradi wa REGROW umefadhili ujenzi wa majengo
mbalimbali katika Hifadhi ya Taifa Ruaha ikiwemo uboreshaji wa viwanja viwili
vya Ndege, kujenga jengo la ikolojia, hostel kwa ajili ya makundi makubwa ya
watalii na kuinua wananchi mbalimbali kiuchumi kupitia vikundi vya COCOBA na
kusaidia wananchi wanaoshi kando ya hifadhi ya Ruaha kukabiliana na Changamoto
ya Wanyama wakali na waharibifu.
Anangisye Mwateba - Hifadhi ya Taifa Ruaha
0 Maoni