Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa 24 ametembelea
kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu cha CURE AFYA kilichopo Kigamboni
jijini Dar es Salaam, na kujionea shughuli za uzalishaji dawa katika kiwanda
hicho.
Akizungumza jana baada ya kushuhudia uzalishaji wa dawa kwenye
kiwanda hicho chenye thamani ya takribani shilingi bilioni 50, Waziri Mkuu
amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji
wanapata faida kutokana na shughuli zao.
“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi wa
miundombinu ya utoleaji huduma za afya nchini, na sasa tunahitaji kupata dawa
na vifaa tiba kwa ajili ya kuendelea kuongeza nguvu kwenye utoaji huduma, hivyo
uwekezaji huu una tija kwa Taifa letu”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji
hao kuendelea kutengeneza dawa zilizo katika ubora unaokubalika katika viwango
vya kimataifa kwenye utoaji wa huduma za tiba.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa kiwanda
hicho kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na weledi ili kumsaidia mwekezaji
huyo kupata faida kutokana na uwekezaji wake.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametembelea
eneo la Dege, Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam kukagua utekelezaji wa agizo
alilolitoa la uwekaji wa taa za Barabarani wakati wa ziara yake aliyoifanya
wilayani humo Oktoba 2024.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni Erasto Kiwale amesema kuwa mpaka sasa taa 67
zimeshawekwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kazi inaendelea.
0 Maoni