Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema uwepo wa mawakala
kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ni kielelezo cha uwazi kwenye zoezi la
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya watendaji wa
uboreshaji wa Daftari ngazi ya mkoa mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema pamoja na
kuhakikisha zoezi linafanyika kwa uwazi mawakala hapo pia watasaidia kuwatambua
wananchi wanaoomba kuandikishwa.
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya
siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. Jambo hili
ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala
hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa
vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia
watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano kama huo mkoani
Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa
(Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amesema katika kuhakikisha zoezi hilo linakuwa
la uwazi Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji
wa Daftari kwa asasi za kiraia 157 na asasi za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi
wa zoezi hilo.
“Ni muhimu kutoa ushirikiano kwa asasi hizo zitakapofika
kwenye maeneo yenu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa
kuwatambua,” amesema Jaji Mbarouk.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya
uboreshaji wa Daftari mkoani Mbeya, Iringa na mkoa wa Dodoma kwenye Halmashauri
ya Wilaya ya Mpwapwa ambapo uboreshaji utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe
27 Desemba, 2024 hadi tarehe 02 Januari, 2025 na vituo vitafunguliwa saa 2:00
asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
0 Maoni