Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa pamoja na jitihada za kuwainua wabunifu wawekezaji nchini, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwawezesha wabunifu wetu kukua zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Desemba 16, 2024 Jijini Dar
es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la Uwekezaji wa Kampuni Bunifu
(STARTUPs).
Amesema kuwa Tanzania imerekebisha mifumo mingi ili
kuwezesha ubunifu na uwekezaji wa moja kwa moja nchini kuleta maendeleo, suala
ambalo tumeona likifanikiwa na kwahiyo linahitaji kupaliliwa na kuungwa mkono kwa
matokeo chanya.
“Nimewasikiliza wanakongamano na kupitia majadiliano haya
ni wazi kwamba bado kuna namna ya kuboresha zaidi mifumo yetu ya usimamizi na
utawala ili kuhakikisha Wabunifu wanapata nafasi nzuri zaidi.” amesema na
kuongeza kuwa, Tunatamani kuona Watanzania wanashiriki katika kukuza uchumi wa
nchi yao na pengine kuazimwa katika nchi nyingine,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema wapo baadhi ya Watanzania wanaofanya shughuli zao nje ya Nchi ambao wanaiwakilisha vema Tanzania kutokana na kufanya kazi kwa kuzingatia misingi iliyowekwa katika nchi hizo na hivyo kuwataka wabunifu wawekezaji kuiga mfano huo.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Maono ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yako wazi na kwa nyakati
mbalimbali amekuwa akijipambanua kuhusu uwezeshaji wa makundi mbalimbali
wakiwemo wabunifu wawekezaji.
“kwa kutekeleza maono ya Rais, ni muhimu kuwasikiliza,
kuwaamini na kufanyia kazi maoni na bunifu zao ili kuboresha mazingira yatakayo
wawezesha kutekeleza Bunifu zao na kupata fursa ndani na nje ya Nchi”.
Naye, Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe.
Stanslaus Nyongo akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Kitila Mkumbo
amesema Serikali imekuwa ikizingatia suala la uwezeshaji kwa Wabunifu
Wawekezaji ikiwa ni pamoja na kupokea maoni yao kupitia Dira ya Maendeleo ya
Taifa 2050.
Nyongo ameongeza kuwa, Serikali imeboresha mazingira ya
biashara kwa kupunguza gharama za biashara ili kuwawezesha wabunifu kutimiza
ndoto zao.
Kwa upande wake, Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mhe. Jerry Silaa amesema Wizara imeandaa mazingira ya kuwawezesha
Wabunifu kufanya majaribio ya kazi zao kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA).
Amesema Serikali imejenga vituo vya ubunifu vinane (8)
katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwawezesha Wabunifu kujiandaa na hatimaye
kupata ajira katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TSA, Zahoro Muhaj
amemshukuru Rais Samia kwa maono yake ya kuwatambua na kuwawezesha wabunifu ili
waweze kuchagiza maendeleo ya nchi.
“ Tunaomba salam zetu zifikishwe kwa Mheshimiwa Rais,
ambaye amekuwa akitubeba na kusafiri nasi katika nchi mbalimbali ili tupate
uzoefu na kukua kama mtu kama mtu mmoja mmoja na baadae kama Taifa,” amesema
Muhaj.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Prof. Nelson Bonephace ameishukuru Serikali kwa jitihada za
kuwawezesha wabunifu wawekezaji kukua.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi sasa zaidi ya
dola za kimarekani Milioni 49 zimetolewa ambazo zinatumika kujenga Kampasi mpya
za Kagera, Zanzibar na Lindi.
0 Maoni