Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amefanya
ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiria na mvua zilizonyesha kwa
siku mbili.
Katika ziara
hiyo Mhandisi Seff alitembelea barabara ambazo zipo kwenye Mradi wa Uendelezaji
wa Miji Tanzania Bara (TACTIC) katika maeneo ya Mkalama, Ilazo, Medeli na
Swaswa-Mpamaa na kubaini mapungufu kadhaa.
Mradi huo wa
TACTIC kwa Mkoa wa Dodoma unajenga barabara Km.10.19 na Mkandarasi 'China Geo Engineering Corporation' ambapo
ilionekana amechelewa kutekeleza mradi huo na kusababisha athari eneo la
Mkalama ambapo kuta za nyumba zimeanguka baada ya mvua kunyesha.
“Hadi sasa
ni zaidi ya miezi 11 tangu aanze kazi hii lakini maendeleo ya kazi ni 35%
badala ya 70%,namuagiza awasilisha mpango kazi
wake na endapo sitoona mabadikiko ndani ya wiki mbili tutachukua hatua za kimkataba.”
Kwa upande
mwingine Mtendaji Mkuu huyo alibaini mapungufu mengine ni kutokuweka tahadhari
za usalama kwa watumiaji wa barabara wakati wa ujenzi kama mkataba unavyotaka.
Hivyo
amemtaka mkandarasi huyo kuweka alama hizo pamoja na kuongeza kasi ya ujenzi wa
barabara hizo kama alivyoagiza la watachukua hatua za kusitisha mkataba wake.
Aidha,
Mhandisi Seff amebaini kuwa kazi za matengenezo za barabara mpya hazifanyiki
kama inavyotakiwa na kwa wakati kinyume na maagizo aliyoyatoa Kwa Mameneja wote
nchi mzima.
“Nasisitiza
kwa Mameneja wote nchi nzima katika kipindi hiki cha msimu wa mvua,mkague
madaraja na mifereji ili kuhakikisha kwamba inapitisha maji kama inavyotakiwa
na kuepusha madhara kwa wananchi na uharibifu wa miundombinu ya barabara.”
Kwa upande
wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Edward Lemelo amesema kuwa wao
kama TARURA Mkoa wameyapokea maelekezo ya Mtendaji Mkuu na kuahidi kuyafanyia
kazi mara moja kwa kuanza na kazi ya uzibuaji wa makavati na mitaro yote yaliyozibwa na takataka ili kuruhusu
maji ya mvua kupita na kuepusha athari kwa wananchi.
0 Maoni