MWENYEKITI
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ‘ameumizwa na kusikitishwa sana’ na tukio la kuuwawa
kwa Ndugu Christina Alex Kibiki, aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo,
mkoani Iringa.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi alipokuwa
akitoa salaam za rambirambi na pole za Mhe. Dkt. Samia wakati wa mazishi ya
Ndugu Kibiki, yaliyofanyika katika eneo la Banavanu, Tosamaganga, Iringa
vijijini, leo Ijumaa, tarehe 15 Novemba 2024.
Ndugu Kibiki
alipoteza uhai usiku wa tarehe 12 Novemba 2024, baada ya kuvamiwa na kupigwa
risasi akiwa nyumbani kwake usiku huo, na watu wambao hawajajulikana hadi sasa,
huku vyombo vya dola, kupitia jeshi la polisi, vikitangaza kuanza kuwasaka kwa
ajili ya hatua za kisheria.
“Nianze kwa
kutoa salaam za pole na rambirambi za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan. Alipokea taarifa za
tukio hili kwa masikitiko makubwa sana.”
“Mwenyekiti
wa CCM ameumizwa na kusikitishwa sana na tukio la mauaji haya ya mtumishi wa
Chama Cha Mapinduzi. Amenituma salaam za pole na rambirambi kwa familia, ndugu,
wanaCCM na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa,” amesema Balozi Nchimbi.
Aidha,
Balozi Nchimbi aliongeza kusema kuwa tukio hilo na mengine ya aina hiyo,
hayakubaliki na yanapaswa kupigwa vita na watu wote ili yakomeshwe mara moja
nchini.
“Kitendo
hiki alichofanyiwa marehemu Kibiki, ambapo mbali ya kumpiga risasi, wakamvunja
mikono yote miwili na kumpiga na kitu kizito, na matendo mengine ya namna hii
hayakubaliki na yanapaswa kukomeshwa mara moja. Yanaleta hudhuni, hofu, mashaka
na kufanya maisha kutotabirika katika jamii ya wataarabu Tanzania,” amesema
Balozi Nchimbi.
Akitoa
salaam za Serikali, Mhe. Peter Serukamba, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa
serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wote waliohusika na
kuhakikisha wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria.
Alisisitiza
kwamba hatua hii ni muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria na kudumisha
amani na utulivu katika jamii.
Aidha, Ndugu
Serukamba alibainisha kuwa tangu tukio hilo litokee, serikali imepokea
ushirikiano mkubwa kutoka kwa mikoa jirani pamoja na makao makuu ya polisi.
Alisisitiza ushirikiano huu umeimarisha juhudi za uchunguzi, na mara tu
uchunguzi utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa kwa umma kwa uwazi na kwa
wakati.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Ndugu Daudi Yasin, ameonyesha imani
kubwa kwa juhudi hizo za serikali, akisema, “Tunajua serikali ina mkono mrefu,
na waliohusika katika tukio hili watahakikisha wananaswa.”
Aidha,
ameongeza kuwa CCM kitaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha
wahusika wanawajibika kwa matendo yao hayo.
Mwenyekiti
huyo pia aliwahimiza wananchi kuwa tayari kuonesha ushirikiano kwa kutoa
taarifa zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kwamba jukumu la kulinda usalama
ni la kila mmoja katika jamii.
Shughuli
hiyo ya mazishi ilitanguliwa na ibada na kuaga mwili wa marehemu Kibiki, katika
Kanisa la Romani Katoliki, Tosamaganga, mkoani Iringa, ambapo misa iliongozwa
na Padri Ernest Magelanga kwa niaba ya Paroko wa Parokia ya Tosamaganga.
0 Maoni