Baraza la
Mawaziri wa Nishati wanaosimamia Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo ambao wanatoka
nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wamekutana na kujadiliana kuhusu mradi
ambao utazinduliwa karibuni.
Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mwenyekiti, Dkt. Doto Biteko amesema
pamoja na mambo mengine wamekubaliana mawaziri warejeshe makubaliano
yaliyofikiwa na Kikao kwa marais ili waridhie uzinduzi rasmi.
“Mradi
umefikia asilimia 99.9 na vimebaki vitu
vichache ili kuukamikisha, katika kikao cha Baraza la Mawaziri kuhusu
mradi tumekubaliana kuwasilisha maombi
yetu kwa wakuu wa nchi ili watakapota nafasi mwakani waweze kuzindua mradi
huu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa
sasa mahitaji ya umeme Tanzania ni Megawati 1,800 na tuna uwezo wa kuzalisha
Megawati 3,070 hivyo kuna ziada ya umeme.
Amesisitiza
“Kuwa na vyanzo vingi ya umeme maana yake tunakuza uchumi wa nchi yetu,
asilimia 52 ya umeme wote tunaozalisha unatumiwa na wananchi na asilimia 48
inatumika kwenye viwanda.”
Dkt. Biteko
ametaja manufaa ya mradi huo kuwa hadi sasa umezalisha ajira kwa watu pamoja na
kusaidia uwepo wa miradi mbalimbali kwa ajili ya huduma kwa jamii hususan
katika Halmashauri ya Ngara (CSR). Aidha, mradi huo umeiunganisha Tanzania Rwanda
na Burundi na pia unatoa fursa ya kuziuzia umeme nchi hizo endapo zitahitaji
licha ya megawati 27 zinazopatikana kwa kila nchi.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko ametoa rai ya utunzaji wa mradi huo ili uweze kuendelea
kutoa umeme “ Mradi huu hauwezi kuwa wa
kudumu kama hatutunzi mazingira na leo tumetoa maelekezo kwa Baraza tuanze kupanda miti katika eneo la mradi ili
kuendelea kutunza mazingira na kuwa na
vyanzo vya uhakika vya umeme.”
Imeelezwa
kuwa, mradi wa huo wa kufua umeme unaotokana na maji wa Rusumo, umeanza
kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa megawati 27 kwa nchi ya
Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha gridi za Taifa za umeme.
Mradi huo
unaotekelezwa na Kampuni ya Umeme ya Rusumo (RPCL) inayomilikiwa na nchi zote
tatu ni kielelezo cha azma ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi
inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za maendeleo na
kijamii.
0 Maoni