Madaktari wa Muhimbili waalikwa Comoro kutoa matibabu ya kibigwa

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Watu wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali ameziomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenda kutoa huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wa nchi hiyo.

Mhe. Ali alitoa  ombi lake hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akiongea na viongozi wa Wizara ya Afya pamoja na wa hospitali hizo katika  mkutano baina yao uliofanyika kwenye  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Waziri huyo wa Ulinzi alisema wataalamu wa hospitali hizo wakienda nchini Comoro licha ya kuwasaidia wananchi kupata huduma pamoja na kubadilisha ujuzi wa kazi na talaamu wenzao lakini pia wananchi wa Comoro watafahamu wakija kutibiwa Tanzania gharama za matibabu zitakuwa kiasi gani na watatibiwa na madaktari gani.

“Tanzania inapata dola za kimarekani milioni 100 kutoka Comoro, hii inaonesha ushirikiano wetu ni wa umuhimu nichukue fursa hii kuwaomba  mfike Comoro ili muone namna ambavyo mtaweza kutusaidia kuwatibu wananchi wetu, pia kuwajengea uwezo wataalam wetu wa afya,” alisema Mhe. Ali.

 Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mhandisi Ismail Rumatila alisema  Tanzania ilitia saini ya ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa Comoro Julai, 2024 katika sekta ya afya ulioruhusu uhamishaji wa wagonjwa kutoka nchini humo kuletwa katika hospitali za afya za umma za Tanzania kwa matibabu.

 “Kupitia ushirikiano huu taasisi zetu za JKCI, MOI na MNH watalazimika kwenda Comoro na kuona namna bora ya kutoa matibabu kwa wananchi na kuwajengea uwezo watoa huduma wa Comoro hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka Tanzania iwe kituo cha umahiri wa tiba utalii barani Afrika,”alisema  Mhandisi Rumatila.

“Taasisi yetu kwa mwaka mmoja imeona wagonjwa 369 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Comoro ni muhimu wacomoro wakatumia huduma zetu za matibabu ya moyo kwani tuna wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kisasa pia mazingira yetu ni sawa na ya kwao,” alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea taasisi hiyo na kusema kuwa JKCI itawatuma wataalam.

Chapisha Maoni

0 Maoni