Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji amebainisha kuwa mafanikio yanayopatikana katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni matokeo ya nidhamu, bidii, na uadilifu miongoni mwa Maafisa na Askari wa Uhifadhi katika kutekeleza majukumu ya Shirika.
Kamishna
Kuji, ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya jana tarehe
12.11.2024 katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara ikiwa na lengo la kuzungumza na
Maafisa na Askari hao waliopo katika hifadhi hiyo.
“Nitoe
pongezi zangu kwa mafanikio ambayo Shirika limeyafikia kupitia hifadhi zake
ambapo Ziwa Manyara ni mojawapo ya hifadhi hizo. Mpaka sasa Shirika limekusanya
zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya mwaka, kwani matarajio yetu mwaka huu ni
kukusanya trillioni na kuondoka kwenye mabillioni. Haya yote ni matokeo ya
uadilifu, nidhamu na kujituma kwa kila mmoja wetu katika kutekeleza majukumu
yetu.”
“Hii ni kazi
kubwa mnayoifanya na ndio kazi tuliyotumwa na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt.Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutii mamlaka ni mwanzo
wa kufungua baraka hivyo nisisitize nidhamu na uadilifu zaidi katika kutekeleza
majukumu ya Shirika.”
Akiwasilisha
taarifa ya hifadhi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dkt. Yustina Kiwango ambaye
ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara alimpongeza Kamishna wa Uhifadhi kwa
kutenga muda wake na kwenda kuwatembelea na kusikiliza changamoto za hifadhi,
Askari na Maafisa wa Jeshi la Uhifadhi waliopo katika hifadhi hiyo. Pia,
ameipongeza Bodi ya Wadhamini TANAPA pamoja na Menejimeti ya Shirika kwa
kuwezesha ufunguzi wa maeneo ya hifadhi ambayo kwa kiasi kikubwa yaliathiriwa
na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuondoa mimea vamizi.
“Niishukuru
Bodi ya Wadhamini, pamoja na Menejimenti ya Shirika kwa mchango mkubwa
mnaotupatia sisi Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara ambapo tumeweza kufungua maeneo
ya hifadhi zaidi ya ekari 400, na kwa sasa watalii wanafurahia kuona ufunguzi
wa maeneo haya ambayo yaliathirika na mabadiliko ya tabia nchi ambapo maji ya
ziwa yalimeza maeneo ya malisho ya wanyama na kupelekea kuwa na wanyama
wachache wanaooneka na uwepo wa vichaka vingi,”alisema Kamishna Kiwango.
Hifadhi ya
Taifa Ziwa Manyara imefanikiwa kufungua maeneo mbalimbali kwa kiwango cha
changarawe ikiwemo eneo la njia panda ya Wayo hadi daraja la Endabashi, eneo la
geti la Mahogan, Majimoto hadi Mto Array, eneo la Migunga ya Nyani, pamoja na
Barabara ya kutoka kituo cha Daudi hadi ATM. Maeneo hayo ya hifadhi ni miongoni
mwa maeneo yaliyoathiriwa kwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Na. Edmund
Salaho- Ziwa Manyara


0 Maoni