Imeelezwa
kuwa uanzishwaji wa Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara (Samia
Infrastructure Bond) unaenda kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo ya
Makandarasi kwa wakati wanapokuwa wamekamilisha kazi.
Hayo
yameelezwa jana Novemba 29 na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini
na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff wakati akitoa taarifa fupi katika
hafla ya uzinduzi wa Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara za Wilaya (Samia
Infrastructure Bond) mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ambaye alimwakilisha Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha,
Mhandisi Seff amebainisha kuwa kuanzishwa kwa Hatifungani hiyo ni muendelezo wa
utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa utekelezaji wa jukumu la
usimamizi, ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara za wilaya zenye
urefu wa Kilomita 144,429.77 ikiwa ni pamoja na madaraja 3,560 pamoja na
makalavati 80,326.
"Changamoto
kubwa tuliyo nayo katika utekelezaji wa jukumu letu ni pamoja na ufinyu wa
bajeti lakini pia uchelewashaji wa malipo ya Makandarasi wanapokuwa
wamekamilisha kazi na hivyo kushindwa kuwalipa kwa wakati kulingana na mikataba."
"Uanziwashwaji
wa Hatifungani hii unaenda kuondoa changamoto hii pamoja na utoaji wa dhamana
za malipo ya awali na utendaji wa Makandarasi na Wahandisi Washauri/Wasimamizi,"
alifafanua Mhandisi Seff.
Hata hivyo,
Mhandisi Seff alieleza kuwa uanzishwaji wa Hatifungani hiyo ni utekelezaji wa
maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyowaasa na kuwashauri TARURA kuwa
wabunifu na kufikiri nje ya boksi ili kukabiliana na changamoto ikiwemo
matumizi ya malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi na matumizi ya teknolojia
mbadala kwa lengo la kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.
Kuhusu
ubunifu, Mhandisi Seff ameongeza kuwa hadi sasa wameweza kujenga jumla ya
madaraja 350 na kilomita 29 za barabara kwa kutumia mawe ambapo gharama
zimepungua kutoka Bilioni 97 hadi Bilioni 30 sawa na asilimia 60.
0 Maoni