Serikali imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau katika kutekeleza dhana ya Afya Moja nchini hasa kwenye maeneo ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi ameyasema
hayo jijini Arusha wakati akifunga mkutano wa afya moja wenye lengo la kupanua
na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta pamoja na taaluma mbalimbali katika
hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na
hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma
mbalimbali katika kutekelezaji wa Afua
hizo.
“Ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana kwa pamoja na wadau
wengine ikiwemo jamii, kwa kuongozwa na wizara za msingi ambazo ni Afya ya
Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi
zote ili kuhakikisha nguvu ya pamoja inatuvusha hapa tulipo na kuendelea kuipa
nguvu dhana ya afya moja,” amesema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi amezikumbusha sekta zote kuendelea kushirikiana
katika kutatua changamoto ya magonjwa ya zoonotiki, usalama wa chakula,
mabadiliko ya tabia nchi na usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndugu Missaile
Musa ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu Mkutano huo wenye tija kwa
Mkoa na Taifa kwa ujumla huku akisema mkutano huo umefanikiwa kukutanisha wadau
kutoka nchi za Kenya, Uganda, Zimbabwe, Namibia, Rwanda, Nigeria, Ghana, Sudan
ya kusini, Cameroon, Senegal, Scotland na Ujerumani na kuwajengea uwezo wa
pamoja na kuweka mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2024 na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 320 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo; Kenya, Uganda, Zimbabwe, Namibia, Rwanda, Nigeria, Ghana, Sudani ya Kusini, Cameroon, Senegal, Scotland na Ujerumani umekuwa ni muhimu sana.


0 Maoni