Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa ujio wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia
ya Kuku na ndege wafugwao kwa Nchi za Kusini mwa Afrika unadhihirisha namna
Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt.
Samia ilivyokuwa na mahusiano mazuri ambayo yamefungua milango katika
sekta mbalimbali ikiwemo ya tasnia ya kuku na ndege wafugwao.
Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo
Oktoba 16, 2024 jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango katika ufunguzi wa
mkutano huo.
Ametaja faida za ufugaji kuku na ndege
wafugwao kuwa ni pamoja na kuchangia usalama wa chakula na kuongeza pato la
Taifa kikanda na kimataifa.
Amesema kuwa asilimia 55 ya kaya
nchini na katika nchi mbalimbali ni ufugaji unaofanywa zaidi na wanawake na
vijana na kuwa Tanzania ina kuku milioni 103.1 wakiwemo kuku wa asili na
kisasa.
Kupitia Jukwaa hilo, Dkt. Biteko
ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha mashamba ya kuku wazazi kwa ajili
ya kuzalisha vifaranga, kuanzisha vituo vya kisasa, maabara pamoja na kuwekeza
katika machinjio ya kisasa ya kuku.
Dkt. Biteko ametoa maagizo mengine
ikiwemo “ Wizara iweke pia mfumo wa mnyororo baridi wa usambazaji wa kuku,
iwekeze pia katika vizimba, chakula cha kuku na ianzishe viwanda vya kusindika
vyakula vya kuku ili vipatikane ndani ya nchi na sio kutumia fedha za kigeni
kuagiza nje.”
Ametoa wito kwa wadau wote wa ufugaji
wa kuku kuendelea kushirikiana na
Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuwa Serikali imetoa fursa kwa kila mmoja kuweza
kujishughukisha na kujiongezea kipato.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko
ameikaribisha sekta binafsi kushiriki katika tasnia hiyo ili kusaidia kukuza
uchumi wa nchi huku akiwataka watafiti kushirikiana na Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya
mkutano wa AGRA uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia
ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa
kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku.
“Tunawashukuru AGRA na Food Alliance
kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika hapa Tanzania na
kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” amesema Mhe.
Ulega.
Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha
kuwa ifikapo 2030 kuku watachangia asalimia 41 ya protini na kuwa watafiti
nchini washirikiane na Serikali wanapotoa matokeo ili kutoleta taharuki kwa
jamii kupitia matokeo ya tafiti zao.
“ Hivi
karibuni watafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya
ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta
taharuki, kupitia Jukwaa hili nitumie fursa hii kuwaambia watafiti washirikiane
na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza
kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa
na kukuza tasnia hii,” amesema Mhe. Ulega.
“Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao
ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa
kufikisha tafiti hizo kwa jamii,” amesisitiza Mhe. Ulega.
Naye, Waziri Mkuu wa zamani wa
Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika
(AGRA), Mhe. Dkt. Hailemariam Dessalegn, amesema kuwa fursa muhimu zilizopo
kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa
vijana na ka kushiriki katika mnyororo wa thamani.
“Jukwaa hili linatoa fursa ya
kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano. Kukuza
tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari wa
wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,”
amesema Mhe. Dessalegn.
Ameongeza “Tanzania ni kinara wa kuwa
na njia shirikishi na ni imani yangu itaendelea hivi chini ya uongozi wa Mhe.
Rais Dkt. Samia ili kufikia ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),
haswa dhamira ya kumaliza njaa na umasikini ifikapo 2030. Hakuna nchi inayoweza
kufikia mafanikio haya peke yake hivyo sera ya ukanda, mafunzo na majadiliano
na mawasiliano ni muhimu kufikia malengo.”
Mfugaji kutoka nchini Malawi, Grace
Gondwe amesema kuwa baada ya kumaliza Chuo Kikuu nchini humo alianzisha
biashara ya ufugaji wa kuku wa kisasa licha ya kukutana na changamoto
mbalimbali amemudu kufanya kazi hiyo kwa miaka mitano sasa na kuwa tafiti
mbalimbali zinaonesha mahitaji yake yaongezeka siku hadi siku.
“Kupitia ufugaji nimekuwa mshauri pia kupitia Kampuni yangu tumeanza kutumia teknolojia katika uzalishaji
wa kuku ambapo uzalishaii umekuwa mkubwa
kwa gharama nafuu. Vijana wenzangu napenda kuwaambia tuendelee kufuga kuku kuna
fursa nyingi pamoja zinazoendana na ufugaji wa kuku,” amesema Grace.
Mfugaji wa kuku kutoka mkoani Tanga,
Bw. Omary Mussa amesema kuwa ameanza ufugaji kupitia miradi mbalimbali na baada
ya mafunzo amekuwa mfugaji tangu mwaka 2023 akianza na kuku 500 na sasa anafuga
kuku 4,000 aina ya chotara na kuku wa kisasa.
“Tanzania kufuga kuku ni utamaduni
wetu tuna kazi ya kubadilisha kutoka kuwa tamaduni kuwa kibiashara nimeanzisha
Kampuni ya Kuku Pesa Investment Group ili watu wafuge kuku kupata pesa,”
amesema Mussa.
Ameongeza “ Changamoto ni kuwa watu
wanafuga bila faida, Kampuni yetu inatoa mafunzo kwa mtu anaye fuga ikiwa ni
pamoja na kubadilisha mitazamo kuwa sio lazima uajiriwe unaweza kujiajiri
mwenyewe. Hadi sasa vijana 108 wamepata mafunzo na ufugaji na tuna wafugaji 98
tunaowasimamia mkoani Tanga.”
0 Maoni