Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewashauri
wabunifu, watafiti, wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, wasanifu majengo na
wajasiriamali kubuni Michoro na Maumbo yenye mvuto na upekee wanayotumia kwenye
biashara zao kama vile vifungashio/mikebe, michoro ili kuvutia walaji na
watumiaji wa bidhaa na huduma na kuhakikisha bunifu hizo zinalindwa kisheria.
Wito huo umetolewa jana na Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa
Mtendaji Mkuu kutoka BRELA katika kikao cha mashauriano ya wadau kuhusu rasimu
ya Mkataba wa Sheria ya Maumbo na Michoro Bunifu iliyoandaliwa chini ya Shirika
la Miliki Ubunifu Duniani (World Intellectual Property Organization-WIPO).
Kikao hicho ni maandalizi ya uidhinishwaji wa sheria hiyo ya kimataifa katika
mkutano wa Kidiplomasia unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2024 Riyadh
nchini Saudi Arabia.
Akifungua majadiliano, Bw. Nyaisa amesema kuwa Mkataba wa WIPO
wa Sheria ya Maumbo Bunifu unalenga kuweka utaratibu au mfumo wa Kimataifa wa
usajili na ulinzi wa Maumbo Bunifu kwa Nchi na Mashirika Wanachama wa WIPO
ambapo mfumo huo utawezesha uwasilishaji wa maombi ya ulinzi wa Maumbo Bunifu
kupitia WIPO ambapo mwombaji ataweza kuwasilisha ombi moja na kuchagua nchi
zaidi ya moja ambazo zitakuwa zimeridhia Mkataba huo ambazo atahitaji kupata
ulinzi wa ubunifu wake.
“Wataalamu wa BRELA wamejiandaa kuwapitisha katika vifungu
vya rasimu ya Mkataba wa Sheria hii ya kimataifa ya maumbo bunifu na
mapendekezo yenu wadau yataboresha sheria hiyo ili itakapopitishwa na Nchi
Wanachama iweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Maoni yenu pia yatatumika
kutengeneza msimamo wa Nchi kuhusu kupitishwa kwa sheria hiyo”, amesisitiza Bw.
Nyaisa.
Ameendelea kusema kuwa, faida za mfumo huu ni kuongeza wigo
wa ulinzi wa Maumbo Bunifu katika nchi nyingi kwa mara moja kupitia WIPO hivyo
kupunguza gharama na ugumu wa ulinzi wa bunifu.
Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, endapo sheria hiyo itapitishwa na
kuridhiwa kwa upande wa Tanzania, itatoa fursa na kuongeza wigo kwa wabunifu wa
maumbo na michoro bunifu kusajili na kulinda bunifu zao katika ngazi ya
kimataifa hivyo kukuza biashara na kuwawezesha kuhimili ushindani katika masoko
ya ndani na nje.
Nae Bw. Mustafa A. Haji, Mrajisi Msaidizi kutoka Wakala wa
Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), akitoa salamu za Mkurugenzi
Mtendaji, amesema kwa upande wa Zanzibar nyanja ya Miliki Ubunifu imekua
kutokana na maboresho mbalimbali ya kisheria na kitaasisi ambayo yameboresha
utoaji wa huduma za usimamizi wa miliki bunifu.
Dkt. Perfect Melkiory, Mhadhiri na Meneja wa Ofisi ya
Usimamizi wa Miliki Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kwa
upande wao wamekuwa wakitoa elimu na usaidizi wa kuandaa maandiko ya bunifu
zinazofanywa na wahadhiri pamoja na wanafunzi ili ziweze kulindwa
Ameendelea kusema kwamba, changamoto iliyopo kwa wabunifu
wengi ni kutokuwa na mwamko wa kulinda bunifu zao mpaka pale wanapogundua
bunifu zao zimeibiwa, na wengine wanarubuniwa kuuza bunifu zao kwa gharama
nafuu kwa kampuni pasipo kujua umuhimu wa kitu alichokibuni.
Maumbo Bunifu ni moja ya nyenzo muhimu za Miliki Ubunifu
inayohusiana na muonekano wa nje wa bidhaa au umbo la vifungashio/vibebeo vya
bidhaa, mikebe, michoro, maumbo ya vito vya thamani, vifaa vya umeme, ubunifu
wa mavazi na alama za picha.
0 Maoni