Katika juhudi za kuboresha uhifadhi wa mazingira nchini,
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
imefanya mkutano na Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) pamoja na
Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo (CBFF) jijini Dodoma.
Mkutano huo umejikita katika kuimarisha mikakati ya pamoja
ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ushirikiano
kati ya pande hizi tatu katika juhudi za kulinda mazingira na kuendeleza
uhifadhi.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa
kikao cha ndani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dk. Pindi Chana
(Mb)anasema mkutano huo unalenga kuimarisha juhudi za kulinda mazingira za
kikanda na kukuza suluhu za pamoja kwa mabadiliko ya hali ya hewa na uhifadhi
wa utofauti wa kibaiolojia katika Bonde la Congo na zaidi.
“Mkutano huu una maana kubwa kwa Tanzania, kama mwanachama
wa CBCC, tunakwenda kunufaika na utaratibu wa pamoja wa usimamizi wa rasilimali
za maliasili, rasilimali fedha, na kuimarisha mifumo ikolojia ya eneo letu
kupitia Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Nchi za
Kati za Afrika (BDEAC) katika kutekeleza makubaliano ya utunzaji Mazingira ya
kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Paris na malengo ya maendeleo
endelevu,”
Aliongeza kuwa kupitia Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo nchi
wanachama 16 zinapata fursa mbalimbali ikiwemo kuandika miradi na kuomba
mashirikiano katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa hasa katika kipindi
hiki ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la watu duniani.
Anasema kutokana na ongezeko hilo la watu duniani nchi
wanachama zimeona kuna umuhimu wa kuungana na kuwa na sauti ya pamoja katika
majadiliano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya
tabianchi, huku zikichangia uzoefu wao na kupokea maarifa mapya kutoka kwa nchi
nyingine wanachama utakaosaidia uboreshwaji wa sera.
Aidha, kupitia mkutano huo wamezungumza mambo kadhaa ikiwemo
namna gani nchi wanachama zinaweza kuendeleza Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo
lakini pia kuongeza uwezo wa wataalamu katika
kulinda mazingira na maboresho ya sera ili mazingira yasiharibiwe.
Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Congo na Katibu
Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC), Mhe. Arlette
Soudan – Nonault anasema pamoja na mambo mengine wamefanikiwa kukubaliana mambo
mbalimbali ikiwemo kujua namna gani wanaweza kuzisaidia nchi wanachama kupata
fedha ambazo tayari zimewekwa katika mfuko wa blue na benki mbalimbali
wanazofanya nazo kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mabadiliko
ya tabianchi.
Aidha, alisema kamisheni hiyo pia itashirikiana na mashirika
mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili kufanikisha dhamira ya kamisheni hiyo na
katika kuhakikisha hilo mwakani kutakuwa na mkutano mkubwa wa wakuu wa nchi kwa
ajili ya kusaidia kamisheni hiyo kufanya kazi huku akisisitiza kuanzisha kwa
redio na luninga itakayofanya kazi kwa lugha nne ambapo nchi wanachama
zitashiriki kutoa maudhui.
Jean Paterne MEGNE EKOGA, Makamu wa Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za
Utawala wa kamisheni hiyo anasema wao jukumu lao kubwa ni kuratibu upatikanaji
wa fedha zitakazozisaidia nchi wanachama na mashirika yasio ya kiserikali
kuisaidia kamisheni hiyo kufikia malengo yake.
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) na mwakilishi wa nchi katika mfuko wa Blue wa Bonde la Congo, Prof. Dos
Santos Silayo alisema kamisheni hiyo ilianzishwa na inaundwa na nchi ambazo
kijiografia, kiikolojia pamoja na kiuchumi zina uhusiano mkubwa katika kulinda
na kuhifadhi bionuai na misitu ya bonde na mito ya Congo, ambayo ina umuhimu
mkubwa katika ustamilivu wa bonde la Congo.
“Tanzania ni nchi ya kimkakati katika kamisheni hii, ujio
huu unalenga kuhamasisha vyombo vya serikali na sekta binafsi ili ziweze kujua
ni nini kinafanywa na kamisheni hii, na ugeni huu utakuwa nchini kwa siku tano
na utakutana na wadau mbalimbali na sisi kama Taifa tumeingia kushirikiana nao
kuimarisha ustamilivu wa rasilimali misitu na wanyamapori,” anasema.
Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo inajumuisha nchi zifuatazo Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kati ya Afrika, Chad, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Guinea Ikweta, Ufalme wa Morocco, Gabon, Kenya, Rwanda, Sao Tome na Principe, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia.
0 Maoni