Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru na kuipongeza Wakala
ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuanza kujenga barabara za zege
kwenye milima mikali iliyopo kata ya Mang’aliza-Kibakwe wilayani Mpwapwa.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati wa ziara ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na TARURA iliyofanywa
na Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi
Rogauts Mativila.
“Niwashukuru sana TARURA na kuwapongeza kwa kutusaidia tulio
kwenye mazingira magumu, jimbo langu la Kibakwe lipo katika maeneo tambarare na
milimani, na hii ni milima mikali ambayo ipo karibu kata sita na hakuna namna
yoyote ya kutengeneza barabara zaidi ya barabara za zege.”
Ameongeza kusema kuwa utaratibu huo wa TARURA wa kujenga
barabara za zege waliouanza miaka
michache iliyopita umeanza kuleta ufanisi mkubwa hususani kufungua maendeleo
pamoja na kuwaletea huduma nyingine wananchi ikiwemo umeme, shule ya sekondari
pamoja na kituo cha afya.
“Kata ya Mang’aliza haikuwa na maendeleo kabisa lakini hii barabara
ilivyofunguliwa hivi karibuni imeleta maendeleo kwa wananchi kwani miaka ya
nyuma nilikuwa nakuja huku kwa pikipiki
lakini sasa hivi nakuja kwa gari na hata magari makubwa yanafika kuleta
vifaa vya ujenzi ambapo kuna shule ya sekondari inajengwa, kwasababu sehemu
korofi zote wameweka zege, kwakweli nawapongeza TARURA,”aliongeza Mhe.
Simbachawene.
“Hata hivyo ombi langu tu waendelee kutenga fedha kwa maeneo
mengine kwani Ilani na sera yetu sasa ni
kuwapelekea umeme na huduma nyingine wananchi lakini changamoto ilikuwa ni barabara ila kusema
ukweli TARURA wamejitahidi sana kwani fedha zinazohitajika ni nyingi ila kwa
hicho kidogo wamefungua hizo njia na zinapitika na shughuli za kijamii
zinaendelea kama kawaida tumeanza kuona tunatokea mahali panapo pambazuka,"
alisisitiza.
Aidha, Waziri huyo alimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuhangaika kutafuta
rasilimali fedha, watendaji wa TARURA kwa kazi nzuri pamoja na TAMISEMI
kwa usimamizi ambapo ana imani nia ya kufungua barabara zaidi itaendelea.
Naye, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus
Mativila amesema mlima huo wenye urefu wa Km. 5 umekuwa mgumu sana kupitika
wakati wa kiangazi na hata masika ambapo chini ya mlima huo kuna uzalishaji mkubwa kutoka kwa wafugaji na
wakulima wa mazoa mbalimbali ambapo TARURA
wameweza kutengeneza maeneo korofi kwa kujenga barabara za zege la
saruji lililochanganywa na kototo pamoja na nondo ambapo hivi sasa barabara
hiyo inapitika.
Mhandisi Mativila amesema kwamba wao kama OR-TAMISEMI wataendelea kuhakikisha mlima huo unaboreshwa na kupitika Ăźmuda wote na kuahidi kuendelea kutoa fedha zaidi ili wananchi waendelee kuzalisha mazao mbalimbali na kupatiwa huduma za kijamii ikiwemo shule na afya.
Na. Catherine Sungura- Kibakwe
0 Maoni