Banda la TAWA lawa kivutio Maonesho ya Kimataifa ya Karibu Kili Fair 2024

  

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amefungua maonesho ya Utalii ya  Karibu Kili Fair 2024 yanayofanyika katika Viwanja vya Magereza Kisongo Mkoani Arusha, yenye lengo la kuitangaza zaidi sekta ya utalii, fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Takribani makampuni 460 ya utalii, yanayotoa huduma katika tasnia ya utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania zikiwemo taasisi za serikali zinazohusiana na utalii ikiwemo TAWA, zinashiriki maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi jana Juni 7, 2024.

Mhe. Kairuki akiambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas alitembelea banda la TAWA na kujionea shughuli za utoaji elimu kuhusu Utalii, Uhifadhi na maelezo kuhusu fursa za Uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

Mhe.Kairuki ameipongeza TAWA kwa kutumia vyema maonesho hayo kwa kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta ya utalii na pia amehasa hamasa zaidi ifanyike katika kutangaza maeneo yote yanayosimamiwa na TAWA ikiwemo maeneo ya Jumuiya ya hifadhi za jamii.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Paul Makonda naye alihudhuria ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Karibu Kili Fair 2024, jana tarehe 07/06/2024 na kupata fursa ya kutembelea pia banda la TAWA, ambalo limekuwa kivutio kwa watu wengi.



Chapisha Maoni

0 Maoni