Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya
ziara ya kikazi katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa lengo la kukagua
miradi ya Sekta ya Madini inayosimamiwa na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO).
Ziara hayo imefanyika leo, Juni 15, 2024 katika mgodi huo
uliopo katika eneo la Kabulo wilaya ya Ileje mkoani Songwe ambapo Kamati hiyo
imekagua miradi mbalimbali katika mgodi huo ikiwemo mradi wa uchimbaji makaa ya
mawe, jengo la uzalishaji mkaa mbadala wa kupikia (Coal Briquettes) na maabara kwa ajili ya makaa ya mawe.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameitaka STAMICO
kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe angalau kufikia uzalishaji wa tani elfu 50
kwa mwezi ili kufikia kiwango kinachoendana na ukubwa wa Shirika.
Aidha, Dkt. Mathayo ameielekeza Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika hilo kuisimamia vyema Menejimenti ya Shirika hususan gharama za
manunuzi ya mitambo na vifaa mbalimbali ili kutoliongezea Shirika mzigo katika
uendeshaji.
Sambamba na hayo, Dkt. Mathayo ameitaka STAMICO kuendelea
kutafuta maeneo mapya yenye hifadhi kubwa na ubora wa makaa ya mawe hususan
katika mikoa ya Ruvuma na Njombe ili kuongeza tija katika uzalishaji wa madini
hayo na kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steve Kiruswa
amesema Wizara ya Madini imepokea ushauri wa kamati na itasimamia vyema
utekelezaji wake ili kuongeza tija na manufaa katika uzalishaji wa madini
nchini.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Vision 2030 itaongeza wigo
kwa watanzania kushiriki katika mnyororo mzima katika Sekta ya Madini
unaounganisha sekta hiyo pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya
wizara likiwemo STAMICO na Taasisi ya
Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa lengo la kuongeza kwenye sekta hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Meja Jenerali (Mst)
Michael Isamuhyo ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kufanya ukaguzi katika eneo la
mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo-Kiwira.
Pia, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Deusdedith Magala
amesema STAMICO inaendelea kuthamini mchango wa Wafanyakazi wake wote katika
kuleta ubunifu na uthubutu jambo lililopelekea Shirika kufanikiwa sambamba na
kuanza uzalishaji wa bidhaa mpya ya Mkaa mbadala wa kupikia ujulikanao kwa jina
la Rafiki Briquette.
Katika hatua nyingine, Magala amesema, kutokana na ukarabati na uwekezaji ulifanywa na STAMICO, mauzo yameongezeka kutoka shilingi 221,389,014 mwaka 2017/18 mpaka 6,144,184, 964.64 katika Mwaka wa Fedha 2022/23 huku Shirika likilipa kodi mbalimbali pamoja na tozo kwa kiasi cha shilingi 950,260,995.87.
0 Maoni