Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wakunga na
wataalamu wengine wa afya nchini kufanya kazi kwa weledi na kuongeza bidii
katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.
Amesema kuwa kada zote za afya zinasimamiwa na miiko na
maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa. "Hivyo basi kila mmoja
ahakikishe anazingatia maelekezo mahsusi ya utendaji wa kazi."
Ameyasema hayo leo (Jumapili, 5 Mei, 2024) alipokuwa mgeni
rasmi katika Siku ya Mkunga Duniani na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakunga
uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC),
jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Wakunga kiwe mstari wa
mbele katika kukemea baadhi ya Wakunga wanaofanya kazi kinyume na maadili ya
taaluma zao.
Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya
kazi kubwa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kutolea huduma ikiwemo
kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kujenga nyumba
za watumishi karibu na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha watoa huduma
wanapatikana wakati wote.
"Serikali imeweka juhudi kubwa katika kununua vifaa
tiba, dawa, pamoja na magari ya kusafirisha wagonjwa ili kurahisisha rufaa kati
ya vituo vya kutolea huduma na wakati inapotokea dharura."
Amesema Serikali imeimarisha mfumo mzima wa rufaa kwa
kushirikiana na wadau unaojulikana kama M-Mama.
Aidha, amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za
kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na
wale wenye matatizo (Neonatal Intensive Care Units) zinajengwa kwenye hospitali
za Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.
"Maboresho hayo yamechangia kuimarika kwa ubora wa
huduma za Afya kwa kuwa yamegusa moja kwa moja mazingira ya kazi ya Wakunga na
watendaji wengine wa sekta ya afya."
Kwa Upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema
Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto
kwa zaidi ya asilimia 80.
"Tunashukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kutuwezesha kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za afya, hususan huduma ya mama
na mtoto, ambayo imetuwezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia
80."
Mheshimiwa Ummy amesema kuwa Serikali imeridhia maombi ya
muda mrefu ya Chama cha Wakunga ya kutofautisha kada ya wauguzi na wakunga.
"Naomba nitoe taarifa kwako tumepokea maoni na ushauri
wa wakunga hususan katika mafunzo ya wakunga ngazi za chini, tunayo changamoto
tunaenda kuibadilisha ili tuanzishe stashahada ya Ukunga."
Awali, Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dkt. Beatrice Mwilike, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya sekta ya Afya ambayo yamewezesha Wataalam wa huduma za Afya kufanya kazi katika mazingira bora.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (kushoto) na rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Dkt. Beatrice Mwilike (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Wakunga Mahiri ambao Waziri Mkuu aliwatunuku vyeti vya kutambua umahiri wao wa kufanya kazi kwa ufanisi katika maafa. Wakunga hao ni Theodora Nakei ( wa pili kushoto) ambaye alifanya kazi kipindi cha maafa ya maporomoko ya udongo eneo la Gendabi wilayani Hanang na Ananyise Makyao ambaye alifanya vizuri katika maafa ya mafuriko Rufiji. Tukio hilo lilifanyika wakati Waziri Mkuu alipofungua Maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijni Dar es salaaM Mei 5, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
0 Maoni