Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Bw. Joshua
Bituri Manumbu ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
kwa jitihada endelevu za kuelimisha jamii namna ya kuepuka madhara yanayoweza
kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko na
kuwadhibiti pale wanapoonekana kuhatarisha maisha ya wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa jana Mei 08, 2024 na Mwenyekiti huyo
katika ziara iliyofanywa na Maofisa wa TAWA wilayani humo.
"Tumekuwa na matukio mbalimbali ya mamba na viboko
kujeruhi watu lakini kupitia elimu inayotolewa na Maofisa hawa wa TAWA na namna
wanavyowadhibiti, wameweza kuokoa baadhi ya watu lakini pia wameweza kuwaondoa
wale wanyama ambao wameshafikia hatua mbaya ya kudhuru watu " amesema.
Katika maelezo yake, Mwenyekiti huyo amesema Halmashauri ya
wilaya ya Ukerewe imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Maofisa wa TAWA kutoka
Kanda Maalumu ya Mwanza na imetoa ushirikiano mkubwa kwa Maofisa hao ili
kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Aidha amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia Maofisa hao vitendea kazi vinavyowafanya
waweze kutekeleza majukumu yao kama sehemu ya taasisi muhimu nchini.
Kwa upande wao,
wananchi wa Kijiji cha Selema kilochopo Kata ya Bwiro wilayani humo
wameipongeza na kuishukuru TAWA kwa elimu wanayoendelea kuitoa wilayani humo
ambayo wamekiri kuwa imekuwa msaada kwao na itawawezesha kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku
wakiepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Selema wilayani
humo, Afisa Habari wa TAWA Beatus
Maganja amesema katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na
waharibifu Serikali inahakikisha usalama wa mwananchi unakuwa ni kipaumbele cha
kwanza na ndiyo maana mara kwa mara Maofisa wa TAWA wamekuwepo maeneo
mbalimbali nchini kutoa elimu na kufanya doria katika maeneo ambayo yanatajwa
kuwa na changamoto ya wanyamapori hao.
Aidha, Maganja ametoa wito kwa wananchi hao kuendelea kufanyia kazi maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu ili waendelee kuwa salama.
0 Maoni