Wadau wa Sekta ya Madini nchini wametakiwa kusoma na kuelewa
mikataba mbalimbali wanayopewa katika makubaliano kabla ya kuisaini hususani
katika taasisi za Bima.
Hayo yamesemwa leo Mei 23, 2024 na Meneja wa Kanda ya
Kaskazini TIRA, Bahati Ogolla katika Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa
Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa
Mikutano AICC jijini Arusha.
Jukwaa hilo linalofanyika kila mwaka limeandaliwa na
Serikali kupitia Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini likiwa na lengo la
kukutanisha wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Madini kujadili na kufanya
tathmini ya ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa sekta hiyo.
Akizungumza Ogolla amesema kuwa, wananchi wengi wanakutana
na changamoto mbalimbali ya mikataba kwakuwa wanaisaini bila kusoma na
kuielewa.
“Someni mikataba vizuri kama huelewi tumia wanasheria au
njoo TIRA kwa msaada zaidi, msiingie mikataba bila kujua faida na
hasara,”amesema.
Amesema kabla ya kuisaini ni vyema kushirikisha baadhi ya
watu ili kushauriana na kuepuka matatizo na maumivu yatakayojitokeza baadaye.
Aidha, TIRA imetoa mapendekezo nane ya kufuatwa ili
watanzania waweze kunufaika na huduma za BIMA.
Mapendekezo hayo yaliyotolewa ni pamoja na
wananchi kuhakikisha shughuli na mali zinawekewa kinga dhidi ya
vihatarishi mbalimbali, kuhakikisha
wanalipa ada za bima inavyotakiwa na
kuhakikisha wanatambua haki na
wajibu wao kwenye mkataba wa bima mfano, ukomo wa muda wa kuwasilisha madai na
uwasilishaji wa vielelezo vinavyotakiwa.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatambua kanuni na
taratibu za bima ikiwemo ulipaji wa ada ya bima, uaminifu uliotukuka, uhusiano
wa umiliki wa mali na mkatabima kurejeshwa kwenye hali iliyokuwepo kabla ya
janga kutokea.
Aidha, ameitaka jamii kushirikiana na mamlaka kufichua vitendo vya udanganyifu kwenye biashara ya bima, mfano, madai yasiyokuwa halali.
0 Maoni