Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza huduma za dharura
zipelekwe kwenye maeneo yaliyopata athari kutokana na kimbunga Hidaya.
Hayo yamesemwa leo (Mei 6, 2024) na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa alichokiitisha
kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwenye maeneo yaliyopata athari.
“Rais ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe katika maeneo
yote yaliyoathiriwa na mvua zilizotokana na athari za kimbunga Hidaya ikiwa ni
pamoja na kupeleka misaada,” amesema. Maeneo yatakayopelekewa misaada hiyo ni
Mafia mkoani Pwani, Kilwa (Lindi) na Ifakara (Morogoro).
Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
lihakikishe linakamilisha zoezi la uokoaji katika maeneo ya Kilwa ambapo zaidi
ya kaya 40 zimezingirwa na maji. “Jeshi la Zimamoto mmefanya kazi kubwa,
hakikisheni maeneo yenye makazi yaliyozingirwa na maji, wakazi wake wanaondolewa
na kupelekwa maeneo salama pamoja na kupewa huduma zote muhimu.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara za Ujenzi,
Uchukuzi, Afya, Maji, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ulinzi na
Fedha zichukue hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna madhara zaidi yanatokea
katika maeneo yaliyopatwa na athari.
“Wizara ya Ujenzi endeleeni kuchukua hatua zote za dharura
zinazohitajika kuhakikisha maeneo ya barabara yaliyokatika yanarekebishwa na
huduma za usafiri zinarudi haraka.”
Waziri Mkuu amepongeza jitihada zinazofanywa na Idara ya
Menejimenti ya Maafa kwa kuendelea kufanya uratibu katika maeneo yote
yaliyoathirika na kuwataka waendelee na uratibu katika maeneo yaliyopata
madhara kuanzia juzi.
“Ongezeni nguvu katika maeneo ya Ifakara, Kilwa na Mafia na
kuhakikisha wananchi wote walioathiriwa wanakuwa katika maeneo salama na
wanapata huduma zote za msingi za kijamii.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Kamati ya Maafa
ya Kitaifa izisimamie Kamati za mikoa na Wilaya ili misaada inayotolewa kwa
waathirika iwafikie walengwa. “Kamati ya Kitaifa izielekeze Kamati za Mikoa na
Wilaya zisimamie misaada yote ya waathirika ili ifike kwa wahusika, baadaye
hali ikisharejea, tutataka tupate taarifa ya kina na jinsi ilivyotumika,” amesisitiza.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni