WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Timu ya Mawaziri
itakwenda wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani kuungana na timu ya watalaam
ili kufanya tathmini ya pamoja kutokana na athari zilizosababishwa na mafuriko
yaliyotokea wilayani humo.
Ametoa kauli hiyo jana wakati wa hafla ya Futari aliyoiandaa
kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Mlimwa jijini
Dodoma.
“Sisi ndio tunaratibu Idara ya Maafa kitaifa, hapa
tunapozungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)
Jenista Mhagama pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonaz wako njiani wanaelekea
mkoani Pwani, mto rufiji umejaa na kata nne zipo kwenye maji, Mawaziri wengine
wa Sekta ikiwemo Afya, Kilimo, Mifugo nao pia wanakwenda ili kuimarisha uratibu
wa zoezi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameipongeza
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namna inavyodhibiti
biashara ya dawa za kulevya nchini.
“Kamishna amefanya kazi nzuri na kuboresha kwenye sekta yake,
hivi sasa Taasisi yake haiishii tu Makao Makuu ya nchi, ameshusha kwenye kanda
na tayari wakurugenzi wameshaenda kwenye maeneo hayo ambao watakamata
wazalishaji, wasafirishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya.”
Viongozi wengine walioshiriki katika iftar hiyo ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mary Maganga na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
0 Maoni