Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema Bwawa la Umeme Julius Nyerere (JNHPP)
halikusababisha mafuriko yanayoendela katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani
Pwani na badala yake bwawa hilo limesaidia kupunguza muda ambao mafuriko hayo
yangetokea kwa kukusanya maji.
Bw. Matinyi amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa
habari jijini Dar es salaam ambapo alieleza kwamba mafuriko hayo yamesababishwa
na mvua za El-Nino ambazo zilianza tangu mwezi Oktoba mwaka jana 2023 na
kuungana na mvua za msimu wa masika mwaka huu 2024, hivyo kusababisha maji kuwa
mengi kuliko msimu wa masika wa kawaida na kwamba hali hii ilitabiriwa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na taarifa hizo zilitolewa kwa wananchi
ili wachukue tahadhari.
“Kutokana na bwawa hili lilijengwa ili lipunguze mafuriko,
mara baada ya kuanza kukusanya maji mnamo Desemba 2022, uwezekano wa mafuriko
ulipungua hadi hivi sasa wakati wa mvua za El-Nino ambapo kiasi cha maji
kimekuwa kikubwa mno. Licha ya kwamba kulikuwa na hatua ya lazima ya kuyafungulia
maji ili kuzuia bwawa lisiharibike, lakini ni hakika kwamba maafa ya mafuriko
yalikuwa yamezuiwa yasiwe makubwa zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Bw. Matinyi.
Amesema kuwa maji yanayopita katika mto Rufiji yalifikia wingi
wa mita za ujazo 8 ,445 kwa sekunde mwezi Februari 2024, na kuendelea kwa
wastani wa mita za ujazo zaidi ya 6500 kwa sekunde, lakini Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) limekuwa likiachia kiwango cha chini kati ya mita za ujazo
3,000 na mara chache hadi 6,000 kwa sekunde kwa siku tofauti za mwezi Machi na
Aprili 2024.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia kamati ya maafa katika kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo Bw. Matinyi alisema viongozi mbalimbali walitembelea maeneo yaliyoathirika ikiwemo wilaya za Rufiji na Kibiti mkoa wa Pwani pamoja na Mlimba wilaya Kilombero mkoa wa Morogoro ambapo walijionea hali halisi na kutoa maelekezo katika huduma muhimu na tayari dawa za tiba kwa binadamu na za tiba ya maji, huduma za afya, chakula, malazi, uokozi, usalama na ushauri nasaha vimeanza kuwafikia wananchi.
Aidha, amesema askari wa wanyama pori wamepelekwa kwenye
maeneo yote ili kudhibiti wanyama aina ya mamba.
“Kwa maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, timu
ya Mawaziri na Manaibu Mawaziri kumi na makatibu wakuu wao, ilifanya ziara
kwenye maeneo yalioathirika mnamo tarehe 10 na 11 Aprili ikiongozwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama
ambao mbali ya kutoa salamu za pole za Mhe, Rais viongozi hao pia walitoa ahadi
za misaada ya serikali na kuagiza miundombinu iliyoharibika ifanyiwe kazi,”
alisema Bw. Matinyi.
Kwa upande wa madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo, Bw.
Matinyi alisema hadi sasa mkoani Pwani kuna vifo vitano (Rufiji 2, Kibiti 2 na
Kisarawe 1) majeruhi 2 Kibiti na 3 Kisaware lakini pia kuna uharibifu wa
mashamba ya mazao yakiwemo mahindi, mpunga, ndizi, ufuta, mihogo, matama na
pamba vilevile makaazi, miundombinu ya barabara, madaraja, nguzo za umeme,
shule, kituo cha afya cha Muhoro kusombwa na maji, jumla watu 126,831
wameathirika mkoani Pwani: 88,768 (Rufiji), 36,900 (Kibiti) na 1,163
(Kisarawe). Hekta za mashamba zilizoathirika ni 33930.24 (Rufiji), 71,366
(Kibiti) na 167 (Kisarawe), hadi sasa Watu 1,014 wameokolewa wilayani Rufiji.
“Mkoani Morogoro zimesababisha vifo 28 katika halmashauri 8 na kubomoa nyumba 1 ,035 zingine 6,874 kuzingirwa na maji. Vifo hivi ni tofauti na vile vilivyoripotiwa na Polisi, vilevile ekari 34,970 za mazao mbalimbali yakijumuisha mahindi, mpunga, ufuta, pamba na mazao mchanganyiko zimeathirika ikiwa ni pamoja na mifugo 1 ,466 imeathirika. Miundombinu ya reli, barabara, makalvati na madaraja imeharibika katika halmashauri za Malinyi, Mlimba, Ifaraka Mji, Ulanga na Manispaa ya Morogoro imeharibika.
0 Maoni