Polisi wachunguza mbunge kushambuliwa kwa risasi

 

Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio la Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mhe. Christopher Ole Sendika kushambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari lake na watu ambao hawajajulikana.

Tukio hilo la mbunge huyo wa CCM kushambuliwa akiwa na dereva wake limetokea jana Ijumaa, katika kijiji cha Ngabolo wilayani Kiteto mkoa wa Manyara wakati Mhe. Sendeka akiwa safarini kutokea Dodoma kwenda jimboni kwake Simanjiro, hata hivyo hawakupata madhara.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime amesema Jeshi la Polisi limepokea taarifa za tukio hilo na wanalifuatilia kwa karibu, ambapo pia uchunguzi wa tukio hilo umeshaanza.

Amesema timu ya wataalamu wa uchunguzi unaohusisha risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, imetumwa kushirikiana na timu ya Mkoa wa Manyara kuchunguza kwa kina tukio hilo, ili kuwabaini wahusika.

Chapisha Maoni

0 Maoni